Rais Samia Suluhu Hassan leo April 26, 2022 ametoa msamaha kwa Wafungwa 3,826 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania, taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ambapo amesema msamaha huo unaenda sambamba na masharti ikiwa ni pamoja na Wafungwa wote kupunguziwa robo ya vifungo vyao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu linalotolewa chini ya kifungu cha 48(1) cha Sheria ya Magereza.
–
Miongoni mwa Wafungwa walioachiwa ni pamoja na waliohukumiwa adhabu ya kifo ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 30 na kuendelea na pia Wafungwa wanaotumikia kifungo cha maisha gerezani ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 20 na kuendelea, pia wanaotumikia adhabu kwa makosa ya kujaribu kuua ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 10 na kuendelea.
–
Wengine ni wanaotumikia adhabu kwa makosa ya usafirishaji na madawa ya kulevya ambao wamekaa magerezani kuanzia miaka 20 na kuendelea na wanaotumikia adhabu kwa makossa ya utekaji au wizi wa watoto ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 10 na kuendelea, pia wanaotumikia adhabu kwa makosa ya wizi au ubadhirifu wa fedha na mali za umma ambao wamekaa gerezani kuanzia mika 15 na kuendelea.
–
Wengine ni wanaotumikia adhabu ya makosa ya matumizi mabaya ya madaraka yao ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka mitano na kuendelea na wanaotumikia adhabu kwa makosa ya utakatishaji wa fedha ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka 20 na kuendelea na wafungwa wanaotumikia adhabu ya makosa ya rushwa ambao wamekaa magerezani kwa kuanzia miaka 10 na kuendelea.