Rais wa zamani wa Kenya, Mwai Kibaki amezikwa leo Jumamosi katika kijiji chake cha Othaya, kwenye kaunti ya Nyeri.
–
Mazishi hayo yamefanyika baada ya ibada ya mwisho iliyoendeshwa kwenye uwanja wa michezo wa Othaya.
–
Akiongoza ibada ya mazishi Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Nyeri, Anthony Muheria, aliwakumbusha Wakenya kuwa Rais Kibaki hakuwahi kumsema yeyote vibaya wakati wowote.
–
Askofu Muheria aliwasihi Wakenya pamoja na waliofika kwenye ibada hiyo kuwa na imani na wepesi wa kusamehe kama alivyokuwa Kibaki.
–
Alisema kuwa Kibaki angewataka viongozi kusita kutoa kauli za uchochezi na badala yake kuhubiri amani.
–
”Tuwe wakweli na wa kusema yaliyo halisi bila ya kuwa jeuri. Tudumishe imani. Hii ina maana pia kuwa wanyenyekevu kwani hicho ni kitu kimoja cha kumuenzi alivyokuwa baba yetu Kibaki. Siku ya leo ni mfano wa jinsi alivyopenda kuishi bila makuu, kwani alitaka afanyiwe maziko ya kawaida,” alisisitiza Askofu Muheria.
Kwenye ibada hiyo, mtoto wa kiume wa Kibaki, Jimmy Kibaki alimsifu baba yake akisema kwamba alikuwa baba ambaye aliyapa uzito masuala ya elimu.
–
Kibaki ameacha watoto wanne na wajukuu kadhaa. Watoto wote walimminia sifa baba yao na kumtaja kuwa mzazi mzuri aliyesisitizia umuhimu wa maadili katika maisha na jamii.