Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa katika kipindi cha robo tatu ya mwaka wa fedha 2021/22, yaani kuanzia Julai 2021 hadi Machi 2022, imekusanya shilingi trilioni 16.69 ikiwa ni sawa na ufanisi wa 97.3% wa lengo la kukusanya shilingi trilioni 17.15.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, makusanyo hayo yaliyokusanywa ndani ya miezi 9, ni ongezeko la shilingi trilioni 3.1 ukilinganisha na kiwango cha makusanyo cha shilingi trilioni 13.59 kilichokusanywa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2020/21, ongezeko ambalo ni ukuaji wa makusanyo ya kodi wa 22.8%.
“Ifahamike kuwa, makusanyo haya kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na kuongezeka kwa uhiyari wa kulipa kodi; kuimarika kwa mahusiano baina ya TRA na walipakodi kunakochagizwa na utatuzi wa migogoro ya kodi nje ya mahakama pamoja na kushughulikia malalamiko ya walipakodi kwa wakati. Pia ufanisi huo umetokana na kuimarika kwa uzalishaji wa viwanda vya ndani na biashara za kimataifa.
“TRA inapenda kutoa pongezi na shukrani za dhati kwa walipakodi wote na wadau mbalimbali kwa kujitoa kwa dhati katika kuendelea kulipa kodi kwa hiyari, kipekee tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa miongozo na msaada wake katika kutekeleza wajibu wetu,” imesema taarifa hiyo.