Shirikisho la Mpira Nchini Ghana (GFA) limeishusha daraja klabu ya Ashanti Gold ya Ghana kutoka Ligi Kuu nchini humo hadi Ligi Daraja la Pili kuanzia msimu wa 2022/23 kutokana na kugundulika upangaji wa matokeo kwenye moja ya mchezo wa Ligi Kuu nchini humo ambapo Ashanti Gold walicheza dhidi ya Allies FC msimu wa 2020/21.
–
Shirikisho hilo pia limeipiga faini ya (GHc 100k) Ashanti Gold ambazo ni zaidi ya Shilingi Milioni 31 za Kitanzania, Rais wao Kwaku Frimpong amefungiwa miaka 10 kutojihusisha na soka na faini ya (GHc 100k) ambazo ni Shilingi Milioni 31 za Kitanzania.
–
Mwanae Emmanuel Frimpong (CEO wa timu) amefungiwa miaka 8 na faini ya (GHc 500k) ambazo ni zaidi ya Shilingi Milioni 153 za Kitanzania, Kocha wao Thomas Duah pamoja na Meneja wa Ashanti Gold, Aidoo Ahmed wote wamefungiwa miaka Miwili ya kutojihusisha na soka kutokana na upangaji wa matokeo.
–
Kwenye video zilizosambaa Mitandaoni zinaonesha Wachezaji wa Allies FC wakijifunga magoli makusudi huku wakionesha kiwango dhaifu sana ambapo Ashanti Gold ilishinda Goli 7-0. Ashantigold ni mabingwa mara nne wa ligi kuu nchini humo.