Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Watu nane wamenusiurika kifo wakati nyumba ambayo wanaishi mtaa wa Mwinamila Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga ikiungua moto na kuteketeza kila kitu ndani. Tukio hilo limetokea leo jioni Jumanne Mei 10,2022.
–
Fred Paulo ambaye ni mtoto katika nyumba hiyo, amesema kuwa ilipofika majira ya saa 11 jioni, alitoka nje kwenda kununua vocha huku simu yake akiwa ameiacha kwenye chaji, aliporudi ndipo akaona moto unawaka ndani.
–
Amesema moto huo ulianza kushika kwenye sofa, ndipo ikabidi akimbie kwenda kuzima umeme (Main Switch), na kuanza kuomba msaada kwa wasamaria wema kusaidia kuuzima moto huo, na kufanikiwa kuuzima huku ukiwa tayari umeshateketeza kila kitu ndani, lakini nyumba yao ikisalimika kuteketea.
“Kwenye hii nyumba tunaishi jumla ya watu nane wakiwamo na wapangaji, na huu moto ulianza kuwaka kwenye chumba changu, nashukuru Mungu nyumba haijateketea yote bali zimepotea samani zote za ndani,”anasema Paul.
–
Naye shuhuda wa tukio hilo la Moto Oscar Kunze, amesema alikuwa amekaa jirani na nyumba hiyo akimsubiri mtu, lakini akasikia kelele nyumba hiyo inaungua moto, ndipo alipofika eneo la tukio na kuanza kusaidia kuuzima, huku watu wengine wakiendelea kwenda na kufanikiwa kuuzima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa huo wa Mwanamila eneo ambalo nyumba imeungua moto Lukia Athumani, amewapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kuokoa nyumba hiyo isiteketee kwa moto, huku akilitupia lawama Jeshi la Zimamoto na uokoaji kwa kuchelewa kufika eneo la tukio, na moto huo kuzimwa na wananchi.
–
Amesema amesikitishwa na Jeshi la Zimamoto na uokoaji kwa kutopokea simu kwa wakati, na baada ya kupata taarifa hawakwenda kwa haraka na kuchelewa kufika eneo la tukio, na walipofika walikuwa wamepanda kwenye bodaboda bila ya kuwa na gari, na kusababisha wananchi kutaka kuwashushia kichapo lakini alizuia tukio hilo.
–
Naye Afisa wa Zimamoto ambaye alinusurika kichapo kutoka kwa wananchi ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema Jeshi hilo linakabiliwa na uhaba wa magari ya kuzimia moto.