Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema kwamba kuanzia Juni Mosi mwaka huu, Watanzania wataanza kupata unafuu katika bei ya mafuta.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Mei 9, 2022, wakati akizungumza na Watanzania kuhusu suala la bei ya mafuta nchini na kusema kwamba kesho Mei 10 Waziri wa Nishati January Makamba, atazungumzia suala hilo bungeni jijini Dodoma.
“Nimeamua wananchi waanze kupata nafuu ya bei ya mafuta kuanzia Juni 1, 2022, nimeelekeza serikali tujibane na tujinyime ili kupata fedha kutoka katika matumizi ya kawaida ya serikali ili ziende kutoa nafuu katika bei za mafuta, kwenye kipindi kuelekea mwaka mpya wa fedha” amesema Rais Samia