Kufuatia kifo cha mwanafunzi wa chuo cha mifugo LITA Morogoro kufariki akiwa anaongelea kwenye bwawa la Mambogo alipoenda kutalii Mkuu wa wilaya ya Morogoro Albert Msando amelazimika kupiga marufuku na kusitisha shughuli zozote za utalii katika vyanzo vya maji hadi pale utaratibu mwingine utakapotolewa baada ya kujiridhisha na shughuli za kiusalama.
–
Mkuu huyo wa wilaya alipiga marufuku hiyo mara baada ya mwanafunzi wa chuo cha Mifugo LITA cha mjini Morogoro John Benako kufariki dunia wakati akiongelea na wenzake wanne kwenye bwawa la Mambogo lililopo mjini Morogoro.
–
Tukio limetokea Mei 15 mwaka huu, na mwili wake kuopolewa Mei 15, ambapo tukio jingine liliripotiwa mwezi uliopita la Mwanafunzi wa chuo kikuu Mzumbe kwa kuangukiwa na jiwe kwenye Milima ya Uluguru wakiwa kwenye shughuli za Utalii.
–
Aidha alisema mwanafunzi Benako alikwenda na wenzake saba maeneo hayo kwa shughuli za Utalii, ambapo wanne waliingia kwenye maji kuogolea huku wakidaiwa kutofahamu mazingira, na ugeni wa lile eneo.
–
” Inadhaniwa akaingia kwenye kina cha maji na kuzama ambapo juhudi za kutafuta mwili wake zilifanyika bila mafanikio siku ya kwanza, Hadi siku ya pili alipoopolewa na askari wa jeshi la Zimamoto na Uokoaji” alisema DC Msando.
–
Hata hivyo alimuagiza mkurugenzi wa Bonde la Maji la Wami-Ruvu kusimamia maelekezo hayo ya kuzuia wananchi kufanya Utalii katika maeneo hayo, hadi pale kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya itakapoweka utaratibu mzuri wakijiridhisha na usalama wa watumiaji wa maeneo hayo ili kuepusha matukio ya watu kufa maji ambayo huenda yakawa ni zaidi hata ya hayo matano yaliyoripotiwa rasmi.