
Rasmi Kocha mpya wa Manchester United, Erik Ten Hag ametambulishwa kwenye dimba la Old Trafford, siku moja baada ya klabu hiyo kumaliza mchezo wao wa mwisho wa msimu dhidi ya Crystal Palace ambapo walifungwa bao 1-0.
–
United wamemaliza kwenye nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, nafasi ambayo inawapa tiketi ya kushiriki michuano ya Europa League msimu ujao.
–
Ten Hag atakuwa na kibarua cha kuhakikisha inairejesha timu hiyo kwenye ramani za ushindani ambapo kwa miaka zaidi ya nane tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson, timu hiyo haikuwa na mafanikio makubwa zaidi ya kubeba mataji matatu ya (FA, Europa na Ngao ya Jamii) wakiwa chini ya Jose Mourinho kati ya 2016-2018.
–
Kocha huyo ameondoka Ajax akiwa bingwa wa Eredivisie (Ligi Kuu Uholanzi) huku akiongoza klabu hiyo kufika hadi nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu wa 2018/19 na hatua ya 16 bora kwa msimu huu. Ameondoka Ajax akiwa na mataji matatu ya Eredivisie kabatini.