Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema kilele cha mashindano ya 67 ya UEFA baina ya Timu ya Real Madrid na Liverpool yataoneshwa mubashara nchini kwenye daraja jipya la Tanzanite jijini Dar es Salaam ambapo vivutio mbalimbali vya utalii vitaonyeshwa kupitia fainali hiyo.
–
Waziri Mchengerwa amezungumza na waandishi wa habari Mkoani Dar es Salaam ambapo amesema mbali na kurusha mubashara mechi hiyo yenye mvuto mkubwa hapa nchini na duniani kote pia filamu ya Tanzania: The Royal Tour itaonyeshwa kabla ya kuanza kwa mechi hiyo ambapo ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
–
Aidha, amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuendelea kutumia sekta za michezo na Sanaa kuitangaza Tanzania na vivutio vyake duniani kwa kuwa zimebeba idadi kubwa ya Tanzania na kuongeza kuwa sekta hizo ndiyo nguvu shawishi ya Serikali zinazowapa watanzania wengi zaidi furaha na faraja.
–
Pia ameongeza kuwa tayari Serikali kupitia kwa Wizara hiyo imekamilisha michoro kwa ajili ya kujenga kumbi za kisasa za michezo na maonesho ya sanaa ambapo ukumbi mmoja unatarajia kuchukua takribani watu elfu ishirini jijini Dar es Salaam na nyingine yenye uwezo wa kuchukua watu elfu kumi na tano jijini Dodoma.