Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi, imetangaza kumsimamisha Mwenyekiti wa chama hiko, James Mbatia pamoja na Makamu Mwenyekiti Bara, Angelina Mtaigwa kwa tuhuma kadhaa zinazowakabili zikiwemo ukiukwaji wa maadili ya chama na kusababisha NCCR- Mageuzi wasishiriki katika mikutano mbalimbali yenye lengo la kujadili masuala ya Demokrasia ya vyama vya siasa nchini.
–
Akitangaza uamuzi huo, Mwenyekiti wa Kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama hicho kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam, Joseph Selasini amesema Mbatia amesimamishwa katika wadhifa huo kutokana na kutokuwa na mahusiano mazuri na makatibu wake ambapo hivi karibuni ziliibuka tuhuma kutoka kwa Katibu Mkuu wa chama, Martha Chiomba akidai kushinikizwa na Mbatia ajiuzulu nafasi hiyo licha ya Mbatia kukanusha tuhuma hizo.
–
Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Sisty Nyahoza ambaye alishiriki katika mkutano huo wa Halmashauri Kuu ya NCCR -Mageuzi amesema ameshuhudia mchakato mzima uliotangazwa juu ya kuondolewa kwa Mbatia katika nafasi ya Mwenyekiti na kuwa wanasubiri taarifa rasmi kutoka ndani ya chama hiko ndipo watatoa msimamo wa ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.
–
“NCCR -Mageuzi walituletea barua kutualika katika mkutano huu na kutuambia kwamba watakuwa na mchakato wa kufanya mabadiliko katika bodi ya wadhamini, pamoja na mabadiliko hayo tukakutana na ajenda nyingine hii iliyojitokeza kuhusu hali ya kisiasa ndani ya chama tukaona amesimamishwa Mbatia na Makamu wake katika uongozi wa chama, tunasubiri taarifa rasmi kutoa NCCR Mageuzi na tutatoa msimamo wa Ofisi ya msajili.
–
Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Uenezi na Mahusiano ya Umma wa Chama hicho, Edward Simbeye akizungumza katika Makao Makuu ya NCCR -Mageuzi baada ya kutangazwa kwa uamuzi huo, amewaeleza waandishi wa habari kuwa mchakato huo uliotumika kumuondoa Mbatia na Makamu Mwenyekiti wake ni batili na kuwa waliofanya hivyo hawana mamlaka, hivyo viongozi hao bado wapo katika nafasi zao kama kawaida.