Katika kuboresha huduma zake na kufikiwa wateja kwa haraka, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limesema linatarajia kuanza kuzipa kandarasi kampuni binafsi kazi ya kuunganisha umeme.
–
Tanesco, katika taarifa yake imesema yenyewe itabakiwa na kazi ya uzalishaji na usafirishaji wa nishati hiyo muhimu.
–
Hayo yalielezwa na Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Maharage Chande na kusema hatua hiyo na nyingize zitasaidia kumaliza tatizo la watu kuchelewa kuunganishiwa umeme.
–
“Watakaopewa kazi ya kuunganisha umeme watalipwa kwa ‘commission’ kulingana na kazi itakayofanywa na tutakuwa tunafuatilia na kubaini iwapo kutakuwa na ucheleweshaji na kuchukua hatua. Lengo ni kumaliza changamoto ya kuchelewa kuunganisha umeme,” alisema Chande bila kufafanua lini hasa wataanza.
–
Hata hivyo, Chande alisema wameanza majaribio na pindi wakapoanza rasmi suala la kuunganishwa umeme litakuwa si shida tena, kwani urasimu utapungua.