Mchungaji Diana Bundala maarufu ‘Mfalme Zumaridi’ na wenzake nane leo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kusikiliza kesi inawayomkabili.
Shtaka hilo namba 11/2022 ambalo ni shambulio la kudhuru mwili linayomkabili kiongozi huyo wa kiroho na wenzake nane limeitwa kwa ajili ya kusikiliza ushahidi huku washtakiwa wakikabiliwa na makosa matatu ambayo ni kumshambulia ofisa wa Polisi, kuzuia ofisa wa Polisi kutekeleza jukumu lake na kumzuia ofisa wa umma kutekeleza wajibu wake.
Baada washtakiwa kufikishwa mahakamani mbele ya Hakimu, Monica Ndyekobora, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Emmanuel Luvinga umemtambulisha shahidi namba moja katika kesi hiyo ambaye ni Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Nyamagana, Christina Mwisongo (46).
Baada ya shahidi kujitambulisha Hakimu alimwagiza wakili wa Serikali, Emmanuel Luvinga kumuongoza shahidi huyo kutoa ushahidi wake huku upande wa Jamhuri ukianza kufanya hivyo.
Baada ya kuulizwa maswali na wakili wa Serikali, Hakimu alitoa nafasi kwa upande wa utetezi kumuuliza maswali shahidi hiyo.
Baada ya pande zote kuuliza maswali hayo kwa saa 2:03, Hakimu aliamuru kesi hiyo iahirishwe kwa dakika 20 kuanzia saa 8:00 mchana huu.