Mwanafunzi anayejiunga na kidato cha kwanza katika shule ya upili ya Kangaru kaunti ya Embu nchini Kenya aliwasili shuleni hapo akiandamana na mamake huku akiwa amebeba kuku kama njia yake ya kulipa karo ya shule ya upili.
–
Kulingana na tovuti ya the Citizen nchini Kenya, Lawrence Murimi, 14, alipata alama 313 katika mitihani yake ya KCPE na kusema alipewa jogoo huyo na mjombake. Akizungumza baada ya kusafiri kilomita 5 hadi shuleni akiwa na mamake, Lawrence aliyekuwa akitokwa na machozi alisema walirudishwa nyumbani kuchukua Ksh.48,000{$480} zinazohitajika kwa ajili ya karo ya shule.
–
“Nilimwambia mama yangu kwamba ni kuku niliopewa pekee ndiye ambaye tunaweza kumpeleka shuleni baada ya kujaribu kugonga milango yote ili kutafuta msaada bila mafanikio,” alisimulia nje ya lango la shule. Aliongeza kuwa kuku huyo alikuwa na thamani ya Ksh.1,000 ikiwa ni fedha kidogo ikilinganishwa karo ninayofaa kulipa katika shule hiyo ili kusajiliwa.
–
Mamake mwanafunzi huyo alisema baada ya kupokea barua ya ksajiliwa kwa mwanawe, alianza kuzunguka afisi zote kutafuta msaada lakini hakufanikiwa. Alisema mwanawe alilazimika kwenda shule ya upili na daftari alizokuwa akitumia katika darasa la nane. Mama huyo kutoka mtaa wa Majengo huko Embu sasa anawaomba wasamaria wema kumsaidia mwanawe.