Na. Najaha Bakari
Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es salaam Alhaji Abduli Maulid amewataka wanariadha wanaokwenda kuiwakilisha nchi katika michezo ya Dunia ya vijana inayoandaliwa na Shirikisho la michezo la Dunia kwa vijana kupambana kwa kutumia maarifa na nguvu zao zote kuiwakilisha nchi kwa ushindi katika michezo hiyo inayoanza kutimua vumbi Mei 14 hadi 22, 2022 nchini Ufaransa.
Ameyasema hayo leo Mei 12 wakati wa kuwakabidhi bendera wanariadha hao watatu huku akieleza kuwa ni zao la mashindano ya michezo, taaluma na sanaa katika shule za msingi (UMITASHUMTA) wakiwemo wasichana wawili Sharifa Mawazo Rashid na Salma Charles ambao wapo kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Filbert Bayi na Ashraka Mahmud kutoka katika Sekondari ya Naipanga ya Mkoani Lindi.
“Nendeni mkajitoe kwa juhudi, maarifa na nguvu zenu zote mkailetee sifa Tanzania, leo mnaondoka hamna kitu lakini tunategemea kuwapokea kitu,”alisema Alhaji.
Kwa upande wake Kocha anayewaandaa katika mazoezi na anayesafiri nao Roberth Kalyahe amesema kuwa wanariadha hao wako vizuri na hakuna mwenye changamoto ya kiafya, ana imani wataenda kufanya vizuri.
Naye Mkuu wa msafara Apansia Lema kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika na wanasafiri leo tarehe 12 na ndege ya saa tisa jioni.
Mashindano hayo yanahusisha michezo tofauti na yanashirikisha mataifa mbalimbali duniani na Afrika,Tanzania ni mara ya kwanza na inapeleka mchezo mmoja.
Serikali ikihusisha Wizara tatu ikiwemo ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Technologia waliyoratibu ushiriki huo wanaendelea na mikakati, mashindano mengine nchi itawakilishwa na michezo tofauti na wachezaji wengi.