Rais Biden na mkewe wakiweka mashada ya maua
Rais wa Marekani, Joe Biden na mkewe, Jill Biden wameenda kuhani msiba mzito wa wanafunzi 19 wa Shule ya Robb Elementary School na walimu wao wawili waliouawa kwa kupigwa risasi na mtuhumiwa Salvador Ramos.
Rais Biden na mkewe wamefanya ziara hiyo Jumapili ya Mei 29, 2022 ambapo wameenda kuweka mashada ya maua kwenye picha za wanafunzi hao kama ishara ya maombolezo katika Jimbo la Texas nchini humo.
Pia inaelezwa kuwa Rais Biden atashiriki ibada ya mazishi ya wanafunzi hao na walimu wao waliouawa na kijana mwenye umri wa miaka 18 aliyevamia shule hiyo akiwa na bunduki na kuanza kufyatua risasi.

Misalaba yenye majina ya wanafunzi waliouawa
Hii ni mara ya pili kwa Rais Biden kuguswa na kuhudhuria matukio ya mauaji makubwa ambapo awali, alifanya ziara katika Mji wa Buffalo, New York ambako mwanaume wa Kizungu akiwa na silaha aliwafyatulia risasi na kuwaua watu 10 weusi kwa sababu za kibaguzi, katika duka moja kwenye mji huo.
Katika mauaji ya wanafunzi hao, vyombo vya usalama vimekuwa vikilaumiwa kwa kushindwa kuchukua hatua haraka kuzuia tukio hilo licha ya kuwa tayari walishapata taarifa kuhusu muuaji huyo.

Rais Biden na mkewe
Inaelezwa kuwa hata wanafunzi waliokwama darasani wakati mauaji yakiendelea walipotoa taarifa kwa polisi, walichelewa kupewa msaada na kuwaweka kwenye hatari kubwa ya kuuawa, jambo ambalo limewaweka polisi katika lawama kubwa.