Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali itaongeza mshahara kwa kutumia utaratibu wa kuwapanga watumishi katika madaraja na vyeo kwa mujibu wa miundo ya utumishi kwa kuzingatia elimu zao pamoja na uzoefu wa kazi ambapo Jumla y shilingi za Tanzania Bilioni 153 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 zimetengwa.
–
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo huko katika viwanja vya Maisara kwenye hotuba yake aliyoitoa ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi), ambapo kwa Zanzibar sherehe hizi zimefanyika Mei 08, mwaka huu, hii ni kufuatia kuwapa wananchi wa Zanzibar muda wa matayarisho ya sikukuu ya Idd el Fitr.
–
Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa ana imani kwamba ongezeko la mishahara litakalofanywa litakuwa na mchango katika kuimarisha uwezo wa watumishi wa umma kujikimu kimaisha pamoja na kuondoa kilio cha muda mrefu kwa watumishi wa umma ambapo elimu na uzoefu wao wa kazi haukuwa ukijitokeza wazi wazi katika marekebisho ya mshahara yaliyofanywa vipindi vilivyopita.