Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza msamaha wa riba iliyotozwa kwa kipindi cha Oktoba 1, 2017 hadi Agosti 31, 2021 kwa waajiri wote waliochelewesha kuwasilisha michango katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
–
Akizungumza wakati wa kutoa msamaha huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa waajiri watakaonufaika na msamaha huo ni pamoja na wale wote waliolipa malimbikizo ya michango wanayodaiwa na WCF na wamebakiza deni la riba pekee.
–
Amesema, waajiri wote watakaolipa malimbikizo ya michango ya miezi ya nyuma wanayodaiwa na Mfuko huo kabla ya Juni 30, 2022 nao pia watakuwa wanufaika wa msamaha huo ambapo hadi kufikia Agosti 2021, takribani waajiri 13,468 wa sekta binafsi na waajiri 191 wa sekta ya umma walikuwa kwenye orodha ya madeni ya riba.
–
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Dkt. John Mduma ameishukuru Serikali kukubali kutoa punguzo hilo kwani linarahisisha usimamizi na utekelezaji wa majukumu ya mfuko huo.
–
Dkt. Mduma amesema anayepaswa kujisajili na kuchangia kwenye WCF ni mwajiri pekee, na viwango vinavyopaswa kuchangiwa ni asilimia 0.6 ya mshahara wa mwezi kwa kila mfanyakazi wa sekta binafsi na asilimia 0.5 kwa mfanyakazi wa sekta ya umma.