Mshambuliaji wa kimataifa wa Senegal anayekipiga Liverpool, Sadio Mane, 30, ataiarifu klabu yake hiyo matamanio yake ya kuondoka msimu huu wa joto. Bayern Munich wanakaribia kufikia makubaliano ya pauni milioni 34 kwa ajili ya kumsajili Mane.
–
Liverpool wamewasiliana na wawakilishi wa winga wa Barcelona Mfaransa Ousmane Dembele, 25. Dembele pia anawindwa na Chelsea. Beki wa Villarreal na Hispania Pau Torres, 25, anakaribia kuhamia Manchester United baada ya wakala wake kusafiri kwenda England kuendelea na mazungumzo ya uhamisho huo.
–
West Ham na Southampton wanafuatilia maendeleo ya mshambuliaji wa Red Bull Salzburg na Austria Junior Adamu mwenye umri wa miaka 20. Leicester City wana nia ya kumsajili kiungo wa kati wa Manchester United Muingereza James Garner baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 kuonyesha kiwango kizuri alipokuwa kwa mkopo Nottingham Forest.
–
Mshambuliaji wa Leeds United raia wa Brazil Raphinha, 25, huenda akapendelea kuhamia Manchester United badala ya Barcelona. Bournemouth na Rangers wanavutiwa na kipa wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England Jack Butland, 29. Aston Villa na Southampton ni miongoni mwa vilabu kadhaa vinavyomwania beki wa Peterborough Muingereza Ronnie Edwards, 19.
–
Tottenham wameiambia Villarreal kuwa wanataka pauni milioni 17 ili kumuuza kiungo wa kati wa Argentina Giovani Lo Celso, 26. Pia Spurs wanakaribia kufikia makubaliano ya kumsajili winga wa Croatia Ivan Perisic, 33, kutoka Inter Milan. Barcelona wanavutiwa na mipango wa kuwasajili mlinzi wa Sevilla na Mfaransa Jules Kounde, 23, au mlinzi wa Napoli raia wa Senegal Kalidou Koulibaly, 30, kama beki mpya wa kati.