Masasi
WAKALA wa huduma za misitu Tanzania(TFS)Kanda ya Kusini imepanda zaidi ya miti milioni 4.3 kuanzia Mwezi Disemba hadi Januari 2022 huku miti milioni 2 ikigawiwa kwa taasisi za Serikali ikiwamo shule na kwa wananchi wa mikoa ya kusini.
Hayo yamesemwa jana na Kamanda wa TFS kanda ya kusini Kamishina msaidizi wa Jeshi la Uhifadhi wa misitu Manyise Mpokigwa,wakati akizungumza na Habarileo ofisini kwake mjini Masasi.
Mpokigwa alisema,kanda ya kusini yenye mikoa ya Lindi,Mtwara na Ruvuma ina mashamba ya miti ambako katika mkoa wa Ruvuma mashamba hayo ni Wino na Mpepo ambako wameotesha miti myepesi inayooteshwa kwa ajili ya kupandwa katika mashamba yao na kugawa kwa taasisi za Serikali.
Alisema, TFS inasimamia aina mbili za misitu ambayo ni miti ya kupandwa na miti ya asili ambapo katika mkoa wa Ruvuma asilimia kubwa ya miti ni ya asili ikilinganishwa na mkoa ya Lindi na Mtwara ambayo miti yake ni ya kupandwa hasa mitiki ambayo inastawi sana katika ukanda wa joto.
Alisema,katika bustani ya miti Ruangwa mkoani Lindi miti iliyozalishwa iligawiwa kwa Halmashauri zote zilizopo katika mkoa huo na wananchi na katika bustani ya Newala mkoani Mtwara miche iliyozalishwa kwa wingi ni ya matunda,miti ya vivuli,mitiki,mkongo na mpingo.
Alisema,TFS inapanda miti kwa malengo mbalimbali kama kurejesha uoto mahali ulipopotea,kubadili mitazamo ya watu kuhusu misitu na miti na wanahimiza jamii kupanda miti ili kupata mazao ya miti toka vyanzo vyao kwa ajili ya kupunguza kutegemea misitu ya asili.
Alisema,wana jukumu la kusimamia na kulinda rasilimali za misitu kwa ajili ya faida ya vizazi vya sasa na vinavyokuja,hivyo ni jukumu ya kila Mtanzania kupanda miti iwe ya mbao,matunda au kivuli kwani kufanya hivyo kutasaidia sana uwepo wa misitu ambayo faida zake ni nyingi.
Alisema,kuna sababu kwa Watanzania kuendelea kupanda miti katika maeneo mbalimbali ili kukabiliana na kasi ya uharibifu wa mazingira inayoendelea kufanywa na baadhi ya watu.
Alisema,mwaka 2020/2021 jumla ya miche ya miti milioni 4 kati ya hiyo miche zaidi ya milioni 2 iligawiwa kwa wananchi na taasisi za Serikali na Dini kama mkakati wa TFS kupanda miti kibiashara.
Alisema, tathimini iliyofanyika imebaini miti mingi iliyogawiwa imeota na michache imeshindwa kuota kutokana na hali ya hewa.
Alieleza kuwa,ile iliyopandwa kwenye taasisi kama shule ilishindwa kuendelea kutokana na janga la Covid-19 ambapo wahudumiaji ambao ni wanafunzi hawakuwepo shuleni hivyo kushindwa kuhudumiwa vizuri.
Alisema,katika kazi zao wanashirikiana kwa karibu na jamii na taasisi za Serikali ambapo mwaka 2021 TFS ilitoa zaidi ya mizinga 50 ya nyuki kwa wananchi katika vijiji mbalimbali ikiwamo kijiji cha Milola.
Alisema, mizinga hiyo imetumika kama sehemu ya kuzuia wanyama waharibifu kama Tembo wanaovamia mashamba na kuharibu mazao na kuvuna asali kwa ajili ya kuwapatia wananchi kipato.
Alisema, katika wilaya ya Songea mkoa wa Ruvuma wamegawa mizinga ya nyuki 100 kwa vikundi vinne vinavyojihusisha na ufugaji nyuki katika maeneo mbalimbali.
Alisema, katika kusaidia maendeleo ya kijamii TFS imetumia Sh.milioni 600 kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii na kutoa vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh.milioni 1.5.
Aidha,mwaka 2022 TFS kanda ya kusini imegawa zaidi ya mbao 200 kwa taasisi za umma ikiwamo shule za msingi na sekondari na miche ya miti kwa ajili ya kurudisha uoto wa asili,kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kuzuia uharifu wa mazingira.
Kamishina Mpokigwa alisema,katika majukumu yao changamoto kubwa ni wananchi kuvamia misitu na kukata miti ovyo bila kufuata taratibu na uchomaji miti moto hasa nyakati za kiangazi,jambo linalo sababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na upotevu wa misitu ya asili.
Pia alisema,uvunaji haramu wa miti unaofanywa na wafanyabiashara wa mkaa wanaotumia baiskeli ambao wanatumia njia zisizo rasmi ni kati ya changamoto kubwa.
Kamanda Mpokigwa,ameziomba Serikali za vijiji na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kusaidiana katika kupambana na uvunaji haramu ya misitu.
“Wananchi wetu lazima wafahamu kwamba misitu ni rasilimali za nchi,hivyo zinapaswa kutumika kwa manufaa ya jamii nzima badala ya watu wachache”alisema Mpokigwa.
MWISHO.