Wafadhili wa kimataifa wamehudhuria mkutano wa sita mjini Brussels wa kuchangisha fedha za kuisaidia nchi iliyoharibiwa kwa vita Syria, wakisema Waysria hawapaswi kusahaulika hata wakati vita vya Ukraine vimekamata hisia za ulimwengu.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema wakati akilifungua kongamano hilo kuwa maoni ya ulimwengu yanaonekana kutoweza kuishughulikia mizozo kadhaa kwa wakati mmoja.
Amekiri kuna aina fulani ya uchovu miongoni mwa wahisani akiongeza kuwa kwa sasa vichwa vya habari vimesheheni tu mzozo wa Ukraine.
Mkutano wa mwaka jana wa wafadhili ulichangisha jumla ya dola bilioni 6.4, ambapo fedha hizo zilitumika kuwasaidia Wasyria na nchi jirani zinazowahifadhi wakimbizi wa Syria na sio kutumiwa na serikali ya Damascus.
Kongamano la leo limezileta pamoja karibu nchi 70 na taasisi za kimataifa yakiwemo mashirika ya Umoja wa Mataifa. Borrell ametangaza euro bilioni moja za ziada kwa mwaka wa 2022.