Dar es Salaam. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (Nimr) ulioangalia uwezo na utayari wa wananchi kulipia bima ya afya ili kufikia malengo ya upatikanaji wa afya kwa wote, umeonyesha asilimia 73 wapo tayari kujiunga na hudma hiyo.
Matokeo ya utafiti huo yataiwezesha Serikali kukamilisha uandaaji wa muswada wa bima ya afya kwa wote (Universal Health Coverage) pasipo vikwazo vya kiuchumi.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema hayo jana, katika ufunguzi wa kongamano la 31 la kisayansi la Nimr lenye kaulimbiu ya ‘Ushiriki wa sekta mbalimbali katika afya, ajenda ya kuimarisha mifumo ya afya kufikia huduma ya afya kwa wote.’
Alisema kati ya Watanzania 10 waliohojiwa kuhusu utayari wao kujiunga na mifuko ya bima ya afya, saba waliridhia pamoja na kuwa tayari kulipia Sh60,000 kwa mwaka ikiwa ni mapendekezo ya Serikali.
Waziri Ummy alisema katika kutatua changamoto ya Watanzania wengi kuwa nje ya mfumo wa bima ya afya, wizara inaendelea na maandalizi ya muswada wenye lengo la kutunga sheria itakayowataka wote kujiunga na bima ya afya.
“Mnatusikia kila siku tunaleta sheria ya bima ya afya itakayokuwa kwa kila mtu na Nimr wameshafanya tafiti imewahoji zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wamesema wana uwezo na wapo tayari kujiunga na bima ya afya kwa sharti walilosema tukijiunga tunaomba dawa zipatikane kwenye hospitali tupate huduma nzuri,” alisema Ummy.
Mbali na ndoto za miaka mingi za Serikali kuanzisha huduma hiyo, imekuwa ikisuasua, hasa kukamilika kwa muswada na kuwasilishwa kwa kamati ya Bunge kabla ya kwenda bungeni kwa ajili ya kujadiliwa kuwa sheria.
Bima ya afya kwa Watanzania wote ilikuwa moja ya ajenda kwa wagombea urais mwaka 2020, huku hayati Rais John Magufuli wakati akifanya kampeni mjini Musoma mkoani Mara akiahidi Serikali itaandaa utaratibu utakaomwezesha kila Mtanzania kupata huduma hiyo muhimu.
Hata hivyo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) imewakusanya watumishi wa umma na wachache walioingia huku jumla yao wakiwa asilimia nane ya Watanzania.
Bima ya Afya ya Jami (CHF) iliyoboreshwa wanufaika wake wengi wapo maeneo ya ngazi za vijiji, kata na wilaya wapatao asilimia 5.4
Kwa bima za afya binafsi, imewakusanya asilimia moja ya Watanzania.
Kwa upande wa NSSF wanufaika waliojiunga ni asilimia 0.3 ya Watanzania.
Hata hivyo, baada ya kuingia madarakani Machi 19, 2021 katika hotuba zake kadhaa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akizungumza kwa kuonyesha nia yake ya kuhakikisha kila Mtanzania anatibiwa, iwe ana fedha au hana fedha kupitia huduma ya bima ya afya kwa wote.
Ili kuonyesha nia hiyo, mwaka wa fedha 2021/22 Sh149 bilioni zilitengwa katika kushughulikia mpango wa bima ya afya kwa wote.
Tangu hapo kulikuwa na danadana nyingi huku wananchi sasa wakiaminishwa muswada ungetua bungeni Novemba 2021 na safari hii aliyekuwa Waziri wa Afya, Dk Dorothy Gwajima aliwahakikishia wananchi kuwa muswada umekamilika.
“Tunatambua kwamba muswada wa bima ya afya kwa wote ni muhimu katika kutatua changamoto za tiba nchini na nikwambie tu tumeshatekeleza maagizo uliyotupatia (Waziri Mkuu) tayari tunasubiri mwongozo wako,” alisema Dk Gwajima mwaka jana.
Hata hivyo, muswada haukuwasilishwa kwenye kamati, kutokana na kusuasua kwa muswada huo na kuwafanya wabunge wacharuke kiasi cha aliyekuwa Spika wa Bunge Job Ndugai kuamua kulivalia njuga.
Ofisa mtaalamu wa uchumi wa afya kutoka Shirika la Afya (WHO), Maximilian Mapunda alisema mfumo uliopo nchini ni wafanyakazi pekee ndio wenye uwezekano wa kuchangia, lakini mfumo wa kodi unaonekana ndio mzuri zaidi kufikia afya kwa wote.
Februari mwaka jana Ndugai alisema, “leteni muswada wa sheria hiyo haraka maana ninyi ndiyo mnategemewa, mkikaa kimya mkisubiri kupangiwa mnaweza kukuta tumemaliza muda wote wa kipindi cha miaka mitano bila sheria kuletwa bungeni na watu wakaendelea kuumia.”
Rais wa Chama cha Madaktari, Shadrack Mwaibambe alisema: “Serikali ikiongeza bajeti kwenye dawa zinaenda ngazi za chini huko ambako kuna gharama nafuu, lakini bado hawawezi kumudu gharama za matibabu.
“Wengi hawajitokezi kutibiwa na wakijitokeza ugonjwa umezidi sana, wengine wanaenda wakiwa na hali mbaya na wengine wanaendea tiba asili,” alisema Mwaibambe.
Hata hivyo, wataalamu na wachambuzi wa masuala ya afya wamesema changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya afya nchini zinategemewa kutatuliwa na uwekezaji fedha.
Wagonjwa wanaotibiwa kwa msamaha wametajwa kuongezeka mpaka kufikia asilimia 70, hali inayochangia vituo vingi vya afya kuishiwa dawa na vifaa tiba, kutokana na kuwa na wachangiaji huduma wachache na wanaotibiwa kwa mfumo wa bima
Akizindua kongamano hilo, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alisema Tanzania inaunga mkono na kuamini katika ufanyaji wa tafiti zitakazokabiliana na changamoto za maradhi.
Alisema mkutano huo ni fursa ya aina yake kwa wanasayansi wa Tanzania kujifunza kutoka kwa kila mmoja na kuunganisha werevu na uwezo katika kupata suluhisho la kimsingi kwa changamoto kuu za kiafya hapa nchini.
Aliiagiza Nimr kuongeza kasi ya ufanyaji utafiti pamoja na kuzalisha chanjo na dawa bora za asili.
Mkurugenzi Mkuu wa Nimr, Profesa Yunus Mgaya alisema chanjo ya Uviko-19 walianza kuifanyia kazi kuanzia Desemba, 2021.
“Tulianza mchakato kujiandaa kufanya utafiti wa chanjo iliyotengenezwa na Watanzania.
“Serikali ilitupatia fedha tuliyohitaji, tuna dozi za kutosha na tunajiandaa kuandikisha watu kwa vituo vya Dar es Salaam na Mbeya, ili tukamilishe ripoti yetu.
“Tunatarajia kukamilisha awamu ya kwanza na kutoa ripoti Desemba. Kama matokeo ni mazuri tutaenda awamu ya pili, tatu na nne na dawa ikionyesha ufanisi tutaiingiza sokoni,” alisema Profesa Mgaya.
Awali, Waziri Ummy alisema wizara itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Nimr ili kutumiza majukumu yao kwa ufanisi.
Alisema tayari Nimr imeshiriki katika tafiti mbalimbali zinazowezesha katika utungaji wa sera na mipango katika wizara ya afya ikiwemo kuwezesha Wizara kupata uhalisia wa utoaji wa chanjo ya HPV ambayo inakinga wasichana dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.