ADVERTISEMENT
Klabu ya FC Barcelona ya Ligi Kuu nchini Hispania ‘LaLiga’ imesaini kandarasi ya miaka minne na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusu masuala ya wakimbizi (UNHCR)
–
Tukio hilo lilifanyika katika ofisi kuu ya UNHCR mjini Geneva, Uswizi na kuhudhuriwa na Rais wa Barcelona, Joan Laporta na Kamishna Mkuu, Filippo Grandi wa UNHCR, viongozi hao wawili waliandamana na Makamu wa Rais wa Taasisi ya FC Barcelona, Elena Fort pamoja na wawakilishi wa Kamati za UNHCR za Hispania.
–
Lengo la mpango huo ni kuongeza uelewa wa sababu ya wakimbizi miongoni mwa mashabiki wa soka duniani kote, huku miradi mbalimbali ikilenga kuboresha maisha kwa watoto wakimbizi na vijana.
–
Miradi hii itazingatia elimu, afya na fursa mbalimbali kwa kuzingatia usawa wa jinsia ili kufikia baadhi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), michezo itatumika kama chombo cha kuwezesha ushirikiano wa kijamii wa wakimbizi.
–
Barcelona Foundation itatoa euro 400,000 kwa msimu kwa miradi yake ya pamoja na UNHCR, ambayo katika msimu huu wa kwanza itafanyika Colombia, Uganda, Uturuki na Malaysia, kwa kiwango cha euro 100,000 kwa kila mradi.
–
Aidha, FC Barcelona watatoa msaada wa vifaa vya michezo vya klabu vyenye thamani ya euro 100,000 kwa msimu na watatoa uzoefu na maarifa ya wataalam wa michezo wa FC Barcelona Foundation kwa ajili ya maendeleo na kukuza amani na mshikamano wa kijamii.
–
Hivyo kwa mara ya kwanza katika historia, nembo ya Shirika la Umoja wa Mataifa itaonekana chini ya namba nyuma ya jezi za Barcelona kwa msimu wa 2022/23.
ADVERTISEMENT