Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewawekea pingamizi mahakamani makada wa zamani 19 wa Chadema na wabunge wa viti maalumu, waliovuliwa uanachama wa chama hicho, waliofungua maombi ya kibali cha kupinga kufukuzwa uanachama wao, huku kikiwasilisha hoja sita.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewawekea pingamizi mahakamani makada wa zamani 19 wa Chadema na wabunge wa viti maalumu, waliovuliwa uanachama wa chama hicho, waliofungua maombi ya kibali cha kupinga kufukuzwa uanachama wao, huku kikiwasilisha hoja sita.
Pingamizi hilo lilisikilizwa leo Jumatatu Juni 13, 2022 na Jaji John Mgetta, ambaye baada ya kusikiliza hoja za pande zote alipanga kutoa uamuzi Juni 22, 2022.
Wabunge hao wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee walifungua maombi Mahakama Kuu, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema, wakiomba kibali cha kufungua shauri la mapitio ya kuhusi uamuzi huo wa kuvuliwa uanachama.
Sambamba na maombi hayo, pia wamefungua maombi ya zuio la muda dhidi ya ubunge wao kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa maombi yao ya kibali cha kufungua kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama wao.
Mdee na wenzake walichukua hatua hiyo baada ya uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema kutupilia mbali rufaa zao za kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho, kuwavua uanachama.
Hata hivyo, leo jopo la mawakili wa Chadema likiongozwa na Peter Kibatala lilishusha hoja sita, ambapo hoja moja ilikataliwa dhidi ya wadai hao.
Hoja hizo ni pamoja na maelezo ya waombaji si halali kwa kusainiwa na mawakili pamoja na waombaji badala ya waombaji tu na sehemu ya uthibitisho kwenye maelezo kwa kusema kuwa wanathibitisha taarifa za kwenye kiapo badala ya maelezo ya waombaji.
Kuhusu viapo, mawakili hao wamesema kiapo kinachounga mkono maombi si halali, kwa kujumuisha maoni na hoja balada taarifa za ufahamu wao na pia kuwepo saini za nawakili kwenye viapo vya waombaji badala la saini za waombaji tu.
Hoja nyingine ni kuishtaki taasisi isiyokuwepo yaani Bodi ya Wadhamini wa Chadema (Bord of Trustee of Chadema), badala ya The Registered Trustee.
Pia wamesema Mahakama haina mamlaka kusikiliza maombi hayo kwa kuiunganisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo haiwezi kuchunguzwa kwa jambo lolote ililolifanya.
Wamesema pia kuwa, Mahakama haina mamlaka kusikiliza maombi ya mapitio ya kimahakama dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema kwa kuwa Chadema si chombo cha umma.
Wameongeza kuwa maombi hayo hayana maana na ni matumizi mabaya tu ya mwenendo wa Mahakama
Hoja zote hizo zilipingwa na wakili wa kina Mdee, Aliko Mwamanenge na Wakili wa Serikali.
Jaji Mgetta pia akiamuru kina Mdee waendelee na ubunge wao hadi tarehe hiyo uamuzi utakapotolewa.
Kamati Kuu ya Chadema iliwavua uanachana Novemba 27, 2020, iliyowatia hatiani kwa kosa la kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum kinyume cha utaratibu wa chama.
Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa ni pamoja na Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnes Lambart, Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.