Na Sweetbetter Njige – TMC Habari.
Mkuu wa wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo amefanya ziara katika kata ya Chamazi, mtaa wa Mbande Magengeni, kwa lengo la kusikiliza kero za Wananchi.
–
Katika ziara hiyo Mhe. Jokate aliambatana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Elihuruma Mabelya, Diwani wa kata ya Chamazi Mhe. John Laurent Gama, wakuu wa idara za manispaa ya Temeke na wakuu wa taasisi mbalimbali za Umma wakiwemo wa TANESCO ,NSSF, Jeshi la Uhamiaji na TARURA,ambapo Wananchi walipata wasaa wa kueleza kero zao na kupata majibu ya kero hizo moja kwa moja.
–
Wakati wa hotuba yake Mhe. Jokate aliwashukuru Wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kutoa kero zao, njia ambayo itasaidia kuboresha hali ya mazingira ya upatikanaji na utoaji huduma.
–
“Changamoto hazikosekani kwenye njia ya kuyafikia maendeleo, nampongeza Mhe. Diwani kwa maendeleo anayoyapata katika kata, shule mpya yenye jumla ya vyumba 20 imejengwa kwa nguvu za Rais wetu Samia Suluhu Hassan.
–
Kupitia ruzuku na mapato ya ndani Mkurugenzi amefanikiwa kutoa milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi Dovya, kupunguza mzigo kwenye shule nyingine, na kituo chetu cha polisi kinaenda kumalizika hivyo tutaimarisha ulinzi,tunatarajia miradi mingi zaidi katika kata hii kama vile kituo cha afya mtaa wa Mkondogwa kinachojengwa kwa milioni 500,TARURA wana mpango wa kujenga barabara za mitaa kwenye kata hii,hivyo tutafanikiwa kupunguza ama kuondoa kabisa kero zilizosemwa hapa kwa kiasi kikubwa”
–
Akizungumza kwa niaba ya Wananchi Mhe. Gama amempongeza Mhe. Jokate kwa kufika kujua hali halisi ya changamoto na kero za Wananchi na kuzitatua.
–
Kwa upande wake mkurugenzi Mabelya amesema kwamba Manispaa imejipanga ipasavyo kuwahudumia Wananchi, na kwamba wasiwe na hofu kwani katika mwaka wa fedha ujao (2022/2023) wamejipanga kuboresha na kukarabati masoko na huduma nyingine mbalimbali ili wakusanye mapato huku Wananchi wakifurahia huduma.