Jeshi la Polisi mkoani Geita linachunguza kifo cha kijana aitwaye Petro Peter (18), mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Dotto Biteko iliyopo kata ya Igulwa wilayani Bukombe aliyekutwa amefariki kwa kujinyonga nyumbani kwao.
–
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa jeshi Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi (ACP) Henry Mwaibambe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lilitokea Juni 4, 2022 ambapo kijana huyo alikutwa amejinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali na tai ya shule.
–
“Huyu mtoto wiki mbili kabla ya tukio hilo la tarehe nne, alikuwa ametoroka nyumbani na kwenda kusikojulikana, wazazi wakatoa taarifa kwa mwalimu mkuu, ambao walianza kushirikiana na mtendaji kumtafuta.
–
“Taarifa ilipofika kwa mtendaji wa Kata ya Igulwa wakaanza kumtafuta huyu mtoto na wakaambiwa atakapoonekana tu huyu mtoto wamujulishe mtendaji wa kata ili waweze kumkamata na kumpeleka shuleni”.
–
“Kwa hiyo mnamo tarehe nne mwezi June, majira ya asubuhi kabisa, huyu mtoto akawa ameonekana hapo nyumbani na wazazi wakaenda kumjulisha mtendaji wa kata kwamba mtoto amesharudi nyumbani.” alieleza.
–
Aliongeza “Baadaye walivyorudi wakakuta tayari huyu mtoto ameshajinyonga kwa kutumia mkanda na tai, hatujui sababu ya yeye kujinyonga lakini vilevile hatujui kwa nini alitoka nyumbani kwa zaidi ya wili mbili zilizopita”.
–
Mwaibambe amesema upelelezi unaendelea kubaini chanzo halisi cha tukio ingawa taarifa za awali zinaonyesha kabla ya tukio hilo kijana alionekana kujihusisha na makundi ya vijana yasiyofaa ambao huenda walimlaghai.
–
Hata Hivyo ACP Mwaibambe Katika maelezo Yake amesema tayari jeshi la polisi limeshakamilisha kufanyia uchunguzi mwili wa marehemu na wazazi wameshakabidhiwa kwa ajili ya mazishi