Benki ya Biashara Tanzania (TCB) inatarajia kutoa gawio la Hisa ikiwa ni sehemu ya faida kabla ya kodi ya bilioni 19.7 kwa mwaka unaoishia Desemba 31, 2021 kulingana na sera na taratibu ambazo Benki hiyo imejiwekea ili kuendelea kuimarisha uendeshaji wake nchini kwa wananchi.
–
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Mkutano wa 30 wa wanahisa wa Benki hiyo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Dkt. Edmund Mndolwa, amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi kubwa iliyofanywa na Bodi ya Wakurugenzi, katika kusimamia Menejimenti pamoja na wafanyakazi, kutekeleza vyema jukumu lake la kusimamia Benki na kuhakikisha ufanisi unaongezeka katika uzalishaji.
–
Dkt. Mndolwa amesisitiza kuwa pamoja na changamoto za mdololo wa uchumi uliotokana na kuzuka kwa wimbi la ugonjwa wa Covid-19 ambao umeleta athari kubwa sana za kiuchumi duniani kote, lakini wameweza kufanya vizuri kwa takribani miaka minne mfululizo kwenye sekta ya benki nchini.
–
Amesema faida hiyo iliyopatikana mwaka 2021, inatajwa kuwa ni kubwa kufuatia ile ya waka 2020, ambayo haijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa Benki ya TCB takriban miaka 95 iliyopita.