Uingereza imesitisha safari ya ndege ya kwanza ya waomba hifadhi iliyokuwa imepangwa kufanyika Jumanne, baada ya Mahakama ya Haki za Binaadamu ya Ulaya kusema mpango huo unaakisi athari zisizoweza kurekebishwa.
–
Uamuzi huo ni baada ya siku kaadhaa za vita nikuvute za kisheria kutoka kwa mawakili wenye kupigania haki za binaadamu, ambao walianzisha mfululizo wa rufaa zenye lengo la kuzuia hatua ya ufukuzwaji watu katika orodha ya serikali.
–
Awali hapo jana maafisa wa serikali ya Uingereza walisema ndege hiyo ingeanza safari yake bila ya kujali itakuwa na abiria wangapi ndani. Lakini baada ya rufaa hizo hakuna aliyesalia. Ijumaa iliyopita vyombo vya habari vya Uingereza viliripoti kuwa watu ambao walipaswa kuondoshwa nchini humo walikuwa zaidi ya 30.
–
Uingereza inajipanga upya kwa safari nyingine. Baada ya kusitishwa kwa safari hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Priti Patel alisema amesikitishwa lakini hana uwezo wa kuzuia haki kutendeka. Hata hivyo amesema timu ya wanasheria ya serikali inapitia kwa kina uamuzi huo na kujiandaa safari nyingine ya ndege.
–
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson aliyekuwa akiukingia kifua mpango huo wa Uingereza anasema kuwa ni njia halali ya kulinda maisha ya watu na kuzuia magenge ya wahalifu ambayo husafirisha wahamiaji kwa kutumia ujia wa bahari wa Uingereza kwa kutumia boti ndogo.