Urusi imeharibu miundombinu ya reli kote Ukraine, jana Jumatatu kwa lengo la kuzuia usambazaji wa silaha za kigeni, huku Marekani ikitangaza kuwa itatoa silaha zaidi licha ya pingamizi la Moscow.
Takriban watu watano wameuawa na 18 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Urusi katika eneo la Vinnytsia, kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine.
Njia za reli pia hutumiwa na raia wanaopita kati ya miji au kujaribu kukimbia maeneo yenye migogoro.
Mapema mwezi huu karibu raia 50 wengi wao wakijaribu kuhamia maeneo salama waliuawa na shambulio la roketi la Urusi kwenye kituo cha reli huko Kramatorsk.
Jana, Jumatatu, mipango ya njia za kibinadamu kuwaruhusu raia kuondoka kwenye kiwanda cha vyuma huko Mariupol ilishindwa.
Moscow ilisema kutakuwa na usitishwaji wa mapigano karibu na kiwanda hicho mapema alasiri lakini naibu waziri mkuu wa Ukraine alisema hakuna makubaliano yaliyofikiwa na kwamba Urusi inafanya kazi bila maafikiano ya pamoja.