CHAMA cha ACT Wazalendo kimeitaka serikali kumrejeshea Wakili Fatma Karume uwakili wake kama sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya kufungua ukurasa mpya ya Rais Samia Suluhu.
–
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu kwenye kikao na viongozi na wanachama wa Kata ya Lilambo, Jimbo la Songea Mjini Mkoa wa Ruvuma jana.
–
Wakili Fatma Karume alifutiwa uwakili wake Mwaka 2019 kutokana na kesi iliyofunguliwa na Ado Shaibu wakati huo akiwa Katibu Mwenezi wa ACT Wazalendo dhidi ya Rais John Pombe Magufuli kupinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Adeladus Kilangi (Miscellaneous Civil Cause No. 29 of 2018).
–
“Mara baada ya kuapishwa, Rais Samia aliahidi kufungua ukurasa mpya wa kisiasa nchini na ameanza kuchukua baadhi ya hatua ikiwemo kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vya upinzani. Bila shaka, kwenu nyinyi wakazi wa Lilambo hatua hii ni jambo lenye maana sana.
–
Ninafahamu hapa Lilambo diwani wa ACT Wazalendo Ndugu Philipo Mhagama alishinda kwa matokeo ya vituoni lakini hakutangazwa. Ninawapongeza kwa mapambano yenu na hatua mlizochukua kupigania haki ikiwemo kulima vibarua mashambani ili kumchangia fedha afungue kesi kupinga matokeo. Hongereni sana” alisema Ado
Credit – Nipashe