ADVERTISEMENT
Na adv. Mussa Makwinya
Nimepata bahati ya kumsikiliza mwamasishaji wa yanga Haji Manara kwenye press yake. Nimesikitika sana kwa baadhi ya maeneo ambayo ameyazungumza kwa hisia na kudhani anaonewa bila ya yeye au washauri wake kumpa ukweli wa mambo. Naomba niweke baadhi ya mambo ambayo naamini hajui atendalo au asemalo.
1) PINGAMIZI NA KESI YA MSINGI KUSIKILIZWA PAMOJA
Katika press yake amesema alishangaa kuambiwa kuwa pingamizi na kesi ya msingi vitasikilizwa pamoja na kusema haiwezekani jambo hilo na hata kwenye mahakama hakuna utaratibu huo. Nilishtuka na kujiuliza kama kweli alikuwa na wanasheria wabobezi kwenye eneo hilo.
–
Na kama anao basi hakufuata ushauri wao. Kimsingi kilichofanywa na Kamati si kigeni kwenye tasnia ya sheria. Upo uwezekano wa kusikiliza pingamizi na kesi ya msingi kwa wakati mmoja na inafanyika mara nyingi mahakamani. Inapotokea hali hiyo, mahakama huanza kutoa uamuzi wa pingamizi (Ruling) na Kisha kama pingamizi halikuwa na mashiko ndipo uamuzi wa kesi ya msingi husomwa (decision).
–
Aidha, endapo pingamizi linakuwa na mashiko hapo ndipo huwa mwisho wa kesi husika. Manara amelishwa matango pori kwenye eneo hilo au amejifanya kujua wakati hajui. Kwa mantiki hiyo, Kamati haikukosea kwenye hoja hiyo ya Manara.
2) KANUNI HAZIJASAJILIWA
Nilitegemea Manara angeueleza umma wa wanamichezo kuwa Kifungu au ibara fulani ya Katiba au Sheria ya BMT inaelekeza kuwa kila kanuni inayotungwa na klabu au Chama cha soka ni sharti kanuni hizo zisajiliwe ili hoja yake iwe na mashiko.
–
Kinyume chake ameleta porojo, ili wanamichezo wasiopenda kusoma na kufanya utafiti waunge mkono porojo hizo. Ibara ya 63(3) ya Katiba ya TFF kinatoa mamlaka kwa Kamati ya utendaji kutunga kanuni zinazoendesha mpira kwa kuzingatia kanuni za FIFA.
–
AIDHA, Sheria ya BMT inazitaka klabu kusajili Katiba zao na hakuna mahali inazitaka klabu kusajili kanuni zao za uendeshaji za kila siku. Kama sheria hiyo ingeweka takwa hilo TFF wangelazmika kufanya hivyo na hoja ya manara ingebeba mashiko. Kinyume chake hakuna kifungu wala kanuni zilizotungwa na sheria hiyo kinchoelekeza suala hilo. Kwa mantiki hiyo na kwa kuwa mpira huendeshwa na TFF kama taasisi huru, hujiwekea kanuni zake na namna ya kuzihalalisha.
–
Madamu yanga na simba ni wanachama, kanuni zao zinapitishwa na Kamati tendaji kwa mujibu wa Katiba ya TFF ambayo klabu hizi ni wanachama. Hakuna asasi binafsi, hata zile zinazosajiliwa Wizara ya mambo ya ndani ambayo husajili kanuni za uendeshaji hadi pale sheria mahsusi inapoelekeza hivyo.
–
Kinachosajiliwa kwa sasa ni katiba zao. Cha msingi kanuni zinazotengenezwa hazipaswi kukinzana na katiba zao na sheria za nchi. Hapa napo Manara ameongea porojo ili apate huruma za watanzania waache kujadili hoja ya msingi ya utovu wake wa nidhamu wake bali tujadili agenda anayoiingiza yeye na ambayo haipo.
3) NAKALA YA HUKUMU
Nikiri kuwa ni haki yake kama mfungwa wa mpira( au moja ya pande ya kesi husika), kupata nakala si ya hukumu tu bali mwenendo ( proceedings) wa shauri lake ili aweze kuifanyia kazi au kujua namna uamuzi wa hoja aliyofungiwa kwayo ulivyofikiwa na kama yale yaliyojadiliwa wakati wa kesi ndiyo yamehusika tu na si jambo lingine.
–
Amedai ameandika kuomba nakala ya hukumu, hata hivyo suala la kupata nakala haulisubiri nyumbani hata kama kwenye mahakama za kawaida. Ni sharti ufuate nakala hiyo na mwenendo mahakamani. Haji hajatuambia lini alienda TFF akataka nakala akanyimwa.
–
Bwana yule anavyopenda media kila mtu angeambiwa kuwa leo naenda. Kimsingi jukumu la kufuata nakala ni la kwake na wala si la TFf kuituma kwake. Ni kweli ameandika barua au kwenda TFF? kama ameweza kutoa nakala ya barua ya Hospitali ameshindwa nini kutuonesha nakala ya barua aliyoipeleka TFF kuomba hukumu? Mbaya zaidi waandishi wa nchi hii walivyotunyima haki hawakuhoji hilo na kupata ukweli. Hapa manara anataka tumwamini yeye na kuipa kasoro TFF wakati hajakidhi kiu ya maswali yetu ambayo waandishi wamekimbia kumuliza.
–
4) SERIKALI IUNDE TUME
Nimesikitika kusikia hoja hii kutoka kwa kiongozi kama yeye. Na kama hizi ndizo hoja za viongozi wa vilabu hivi, hasa yanga anayoitumikia basi tunayo safari ndefu kufikia mafanikio ya soka.
–
Anajua vipo vyombo vya haki ambavyo anapaswa kuwasilisha hoja zake na bado hajafanya hivyo. Tume ya nini wakati bado vipo vyombo vya haki hajavifikia? Kwa mantiki ya hoja hii ndiyo maana hataki kwenda kuchukua nakala ya hukumu yake.
–
Nimejiuliza, Tume ikachunguze nini? Matusi au hoja gani na kwa maslahi ya nani, je yeye ni mtu maalum kwenye tasnia ambaye akiguswa tu serikali iamke? Alikuwa na mawakili wake kwanini hawakuwasilisha hoja alizonazo wakati wa shauri? Nini maana ya kuwa na wakili? Naomba kwa ajili ya muda niishie hapa.
ADVERTISEMENT