Mahakama ya Wilaya ya Ludewa imemhukumu kifungo cha miaka 5 jela John Chale (60) mkazi wa kata ya Ilela wilayani Ludewa mkoani Njombe kwa kosa la kumfanyia vitendo vya kishirikina mtoto wa mdogo wake Videana Chale (18) na kupelekea kupata ukichaa.
–
Akisomewa hukumu hiyo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya Ludewa Isaac Ayengo imeelezwa kuwa binti huyo alipatwa na kichaa ambapo wazazi wake walimpeleka kwa mganga wa kienyeji ndipo walipoambiwa kuwa amerogwa na mshtakiwa huyo lakini hawakuishia hapo walimpeleka kanisani nako ikagundulika hivyo pia ndipo walipoamua kumuuliza mshtakiwa huyo kwakuwa amekuwa na tabia ya vitendo vya kishirikina na anamiliki Nyoka ndani ya nyumba yake ambaye kwa macho ya kawaida amekuwa akionekana kama jiwe.
–
Aidha mshtakiwa huyo alikiri kutenda kosa hilo ndipo baba mzazi wa mtoto huyo Hekima Chale akaamua kupeleka jambo hilo katika vyombo vya sheria ambako mtuhumiwa huyo alikana lakini baada ya kufanyika upelelezi na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili mahakama ilijilidhisha kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo pasipo shaka yoyote ikiwa ni kinyume cha kifungu namba 3(a) na 5(1) cha sheria ya uchawi sura ya 18 marejeo ya 2019.
–
Hata hivyo Mwendesha mashtaka wa serikali Asifiwe Asajile aliiomba mahakama kumpatia mshtakiwa huyo adhabu kali ili iwe fundisho kwake na kwa jamii kwani vitendo vya kishirikina vimekuwa vikisababisha migogoro katika familia na jamii kwa ujumla ndipo mahakama hiyo ikatoa hukumu ya kifungo cha miaka mitano jela.
–
Kwa upande wa utetezi wake mtuhumiwa huyo aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu hiyo kwakuwa ni kosa lake la kwanza, anategemewa na familia na pia ni mgojwa wa kisukari lakini mahakama ilimtaka kutumikia kifungo hicho.