
RAIS Mhe.Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo 10 kwa watendaji wa OR-TAMISEMI na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA), huku akiagiza Wakandarasi wababaishaji wasipewe kazi za ujenzi wa miundombinu.
Pia ameitaka TARURA kuratibu miradi mingine ya miundombinu inayojengwa Mijini na Vijijini ikiwamo ya mradi wa uboreshaji miundombinu kwenye Miji na Majiji (TACTIC) na Mradi wa uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP).
Mhe.Samia ametoa maagizo hayo jana jijini Dodoma kwenye hafla ya kusaini mikataba 969 yenye thamani ya Sh.Bilioni 331.39 ya ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na TARURA kwa mwaka 2022/23.
Amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TARURA awasilishe kwa Bodi ya Usajili ya Wakandarasi na Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA) orodha ya wakandarasi walioonesha ubabaishaji ili wasipewe tena kazi maeneo mengine wakaendelea kuharibu.
Aidha, ametaka TARURA isiingie makubaliano na mkandarasi yeyote kabla ya kujiridhisha uwezo wa kutimiza makubaliano ya mkataba wa ukandarasi.
Kadhalika, ametaka mikataba hiyo iliyosainiwa kutokwenda mikononi mwa madalali bali iende kwa wakandarasi wenye uwezo na vigezo stahiki.
Amesisitiza Wakala huo kuwa na mipango ya muda mfupi na mrefu na taratibu zote za kuanzisha miradi zianze mapema na kwa uwazi ili kuepuka migongano ya kimaslahi.
Amesema utekelezaji wa maagizo hayo yatakuwa ni kipimo cha TARURA kuongezewa fedha za kutimiza majukumu yake.
Alihimiza matumizi ya teknolojia mbadala ili kuboresha barabara za vijijini na kuondokana na mchanga na changarawe.
&&&&&


