
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewataka wananchi wote waliovamia na kujenga kwenye maeneo ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) eneo la Kigamboni kushirikiana na mfuko huo kwa kukubali kulipa fidia ya fedha, ili waweze kumilikishwa na kuendelea kusalia kwenye maeneo hayo.
Makalla ametoa maelekezo hayo Kufuatia kamati iliyoundwa kuchunguza mgogoro huo kubaini wananchi hao walivamia maeneo ya NSSF na kujenga kinyume na sheria.
Akizungumza na wavamizi hao wakati wa ziara ya utatuzi wa migogoro ya ardhi wilayani Temeke, Makalla ameelekeza NSSF kurasimisha upya maeneo hayo kwa kupima viwanja, ili wavamizi walio tayari kulipa walipe na baada ya mgogoro kuisha wananchi watapitiwa na zoezi la anuani za Makazi na kupatiwa namba.
Mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salaam amesema, maamuzi hayo ni sehemu tu ya busara ya serikali na ameonya tabia ya wananchi kuvamia maeneo ya watu na taasisi.