
Naibu Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) Taaluma, Utafiti na Ushauri Dkt. Michael Msendekwa amesema dhumuni kubwa la ujio wa wageni wa Chuo hicho kutoka Nigeria ni kujifunza masuala ya Serikali za Mitaa.
Dkt.Msendekwa ametoa kauli hiyo hivi leo Jijini Dodoma wakati baada ya kutoa mafunzo kwa wageni hao ambao wamekuja kujifunza kuhusu uendeshaji wa Serikali za Mitaa nchini.
“tunawaelezea habari ya uendeshaji wa Serikali za Mitaa kwa ujumla kwa Tanzania na tunawaonyesha jinsi gani tunawezesha Serikali za Mitaa kufanya kazi lakini pia tunabadilishana uzoefu katika mambo ya Uongozi,” amesema Dkt Msendekwa
Mbali na kujifunza masuala yanayohusu Serikali za Mitaa nchini Tanzania wamepata fursa ya kufanya ziara kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, kutembelea Ofisi za Jiji la Dodoma na baadhi ya miradi yake.
Dkt. Msendekwa amesema, wageni hao wanatokea kwenye Taasisi inayojulikana kama ‘Institute Of Policy and Strategic Studies, Kuru Nigeria’, na lengo ni kujifunza kuhusiana na mambo ya Serikali za Mitaa hivyo wao kama chuo cha Hombolo wapo kwa ajili ya kuwezesha masuala mbalimbali kuhusiana na historia za Serikali za Mitaa na pia watapata fursa ya kutembelea kijiji cha Mnenia kilichopo Wilayani Kondoa mkoani Dodoma.
“kesho tutawatembeza katika vijiji vingine kwa mfano Kondoa katika kijiji cha Mnemia na kuonyesha ni jinsi gani mchakato wa fursa za kimaendeleo unavyofanyakazi” Alisema Dkt. Msendekwa.
Naye Profesa Ibrahim Dinju Choji Mni amesema kuna changamoto nyingi ambazo zipo kwenye Serikali za Mitaa nchini Nigeria ambazo nilianza kufanyiwa maboresho kuanzia mwaka 1996 lakini bado wanaendelea kuzitatua na sasa watapata historia nzuri na uzoefu wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo juu ya namna ya kupanga mipango ya Utawala katika Serikali za Mitaa ambayo itasaidia kwenye majimbo yao.
Wageni hao ambao ni Wataalam na Viongozi huagizwa na Rais wa nchi yao kutembelea nchi mbalimbali kujifunza namna ya nchi nyingine zinavyofanya kazi katika Sekta tofauti na kwamba timu ya ugeni kama huu imekwenda nchini Uganda, Cameron na Ethiopia.



