
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka wataalamu kutoka mtandao wa haki za kisheria kuwasilisha rasmi andiko la mapendekezo ya maboresho ya Sheria mbalimbali zinazohusu ukatili wa kijinsia kwa watoto ili kuja na Sheria moja itakayokidhi mahitaji ya sasa.
Akizungumza na wataalamu hao jijini Dar es salaam Agosti 29, 2022, Waziri Gwajima amewapongeza kwa hatua ya kuandaa andiko hilo, linalokwenda sambamba na mpango wa Serikali kupitia wizara za kisekta la kufanyia kazi maboresho ya sheria zinazohusu ukatili wa kijinsia na dhidi ya watoto.
Amewataka wanamtandao hao kuwasilisha rasmi andiko lao Wizarani Ili mapendekezo hayo yaingie kwenye utaratibu rasmi unaoendelea kupitia kikosi kazi cha wataalamu wa kisekta.
Dkt. Gwajima amesema agenda hiyo ni muhimu na kama ilivyojitokeza kwenye michango ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati alipowasilisha hotuba ya bajeti ya wizara mnamo tarehe 30 Mei, 2022.


ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT