Watu 27 wamefariki dunia na wengine 20 wamejeruhiwa baada ya basi lililokuwa likiwapeleka kwenye kituo cha karantini ya Uviko19 kupinduka katika jimbo la Guizhou nchini China.
–
Ajali hiyo imeamsha hasira kali mitandaoni kutoka kwa wale wanaoikosoa sera ya Uviko19 ya China.
–
Sera hiyo inahusisha watu wengi kupimwa na kufuatiliwa. Wale wanaokutwa na virusi vya ugonjwa huo pamoja na watu wao wa karibu hutakiwa kujitenga nyumbani au kwenye vituo vya karantini.
Wakati dunia ikijaribu kuishi na Uviko19, China ndio nchi pekee kubwa ambayo bado inaipa kipaumbele vita dhidi ya virusi hivyo.
–
Mamilioni ya watu hupanga foleni kupimwa ugonjwa huo kila baada ya siku tatu ili kuweza kupata ruhusa ya kuingia kwenye majengo ya umma na hata baadhi ya maduka.