


Dar es Salaam, Septemba 21, 2022: Benki ya Stanbic Tanzania imetilia mkazo dhamira yake ya kusaidia wajasiriamali wadogo na wa kati kwa kutoa huduma zinazokidhi mahitaji yao na kutatua changamoto zinazowakabili. Ahadi hiyo ilitolewa na Mkuu wa Incubator wa Benki ya Stanbic, Kai Mollel, wakati wa Kongamano la 6 la mwaka la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lenye kaulimbiu: “Uwezeshaji wa Watanzania katika Uwekezaji’’ lililofanyika Septemba 19, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa LAPF, Dodoma huku benki hiyo ikiwa ndiyo mdhamini mkuu.
Jukwaa hilo la siku moja lilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Muungano Jamhuri ya Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ambaye aliwapongeza wadhamini wakuu kwa kuisaidia NEEC kufanikisha jukwaa hili, huku akitilia mkazo kuwa serikali inathamini mchango wao kwa kuzingatia kwamba serikali iko katika mpango wa kutengeneza mazingira mazuri ili watanzania waweze kushiriki katika shughuli za uwekezaji.
Wakati wa hotuba yake, Mollel aliahidi kuwa benki itafanya kazi bega kwa bega na serikali katika kusaidia ukuaji wa wajasiriamali. “Tunapenda kuihakikishia serikali, wafanyabiashara na wadau wote wa maendeleo kwamba sisi kama benki tutaendelea kushirikiana nanyi katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu.” Mollel alisema
Aidha aliipongeza NEEC kwa kuandaa kongamano hilo huku akiweka wazi kuwa benki hiyo imefurahi kuwa sehemu ya mazungumzo yatakayochochea uwekezaji wa ndani (Local content). “Benki yetu inaongoza kwa uwekezaji, na mwaka huu tumetunukiwa tuzo ya Benki Bora ya Uwekezaji na EuroMoney Market Leaders kwa mwaka 2022 kutoka kwa jarida la EuroMoney. Hii ni kwa sababu tumeendelea kutoa huduma mbalimbali zinazowawezesha watanzania kushiriki na kunufaika na uwekezaji nchini.” alisema Mollel
Benki ya Stanbic imekuwa katika safari ya ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati, na hivi karibuni imeingia ubia na NEEC kutekeleza programu ya Supplier Development ambapo wajasiriamali watapatiwa mafunzo na kupatiwa vitendea kazi vya kuwawezesha kutumia fursa za uwekezaji nchini na kuongeza ushindani wao kikanda na kimataifa.
Benki ya Stanbic inaendelea kupiga hatua katika kukuza uwekezaji miongoni mwa wateja wake nchini. Kuunga mkono jukwaa hili ni ishara kuwa benki imejidhatiti kuimarisha sekta ya uwekezaji, pamoja na kuwawezesha wananchi kutumia rasilimali na fursa zilizopo ili kuleta maendeleo ya kiuchumi katika taifa hili.
End.