
Dar es Salaam, Septemba 28: Benki ya Stanbic Tanzania, imezindua rasmi huduma maalumu kwa ajili ya wajasiriamali wadogo na kati, iitwayo ‘Mpambanaji’, inayobeba kauli mbiu: Tunakuwezesha Kukuza Biashara Yako. Huduma hii mpya inalenga kuwezesha wajasiriamali kufikia Huduma za kibenki kirahisi, ili kufikia fursa za uwekezaji nchini na kuongeza ushindani wao wa kikanda na ulimwengu.
Mpambanaji ilizinduliwa katika kampeni iliyoambatana na mkutano na waandishi wa habari pamoja na warsha iliyoandaliwa kwa wajasiriamalii ambayo ilifanyika katika hoteli ya Goldcrest jijini Mwanza.
Mpambanaji inajumuisha huduma mbalimbali, ambazo ni; Akaunti mahususi kwa wajasiriamali (akaunti ya Mpambanaji mmoja mmoja, Vikundi, na Saccos), Huduma ya Stanbic Biashara incubator (programu inayolenga kujenga uwezo/kuelimisha), Huduma za kibenki bila mipaka (borderless banking), mikopo ya vyombo vya usafiri, huduma za Bima, Huduma ya kufanya biashara kati ya Tanzania na China, pamoja na huduma mpya ya Wakala wa Benki (Stanbic Wakala) yenye zaidi ya mawakala 500 wanaoongeza uwepo wa huduma za benki nchini.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Mkuu wa Kitengo cha Biashara, Fredrick Max, amesisitiza kuwa Mpambanaji inakusudia kutatua changamoto zinazozuia wafanyabiashara kufikia malengo na kufanikiwa, ikiwemo kurasimisha biashara zao ili kuwaunganisha na Huduma za kibenki.
“Sekta ya Biashara ndogo na kati ni zaidi ya 70% ya sekta binafsi na inatoa ajira kwa zaidi ya watu milioni 4, kwahiyo ina mchango mkubwa katika kuchangia uchumi wa Tanzania ikiwa zitarasimishwa”. Alisema “Ndio maana kama taasisi ya fedha tumetambua umuhimu wa kuleta suluhisho ambalo ni zaidi ya usaidizi wa kifedha, kwa kuja na suluhisho ambalo litahakikisha wafanyabiashara wana zana wanazohitaji ili kuanzisha biashara endelevu na zenye faida” Max alieleza.
Mkuu wa Kitengo cha wateja binafsi, Omari Mtiga aliweka wazi kuwa benki itaendelea kutafuta ufumbuzi pamoja na kubuni huduma zitakazokidhi kiu ya wateja wao. “Akaunti ya Mpambanaji ni ya wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao wanahangaika kila siku ili kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kibiashara. Benki ya Stanbic iko hapa kukusaidia katika safari yako ya mabadiliko,” Alisema Mtiga.
Aliongeza kwamba wajasiriamali wanaweza kufungua akaunti ya Mpambanaji kwa kutumia TIN namba pamoja na kitambulisho cha taifa (NIDA). Vilevile, akaunti hii haitakuwa na ada ya mwezi na kupitia akaunti hii mteja ataweza kuweka fedha, kutoa fedha na kufanya malipo.
Kama sehemu ya uzinduzi, benki ikishirikiana na wadau kama BRELA, Serikali za Mitaa na TRA waliandaa warsha maalumu kwa wajisiriamali jijini Mwanza.
Mkuu wa Incubator, Kai Mollel aliweka wazi kuwa warsha hii itaendelea katika mikoa mingine pia ikiwemo Arusha, Mbeya, Tanga na Dar es Salaam kama sehemu ya huduma za benki yenye lengo la kuinua wajasiriamali ili kuwawezesha kukuza biashara zao. “Lengo letu ni kuona kila ‘Mpambanaji’ anafanikiwa”. Alisisitiza Kai.
Kiwa kama benki yenye tuzo ya Benki Bora ya Uwekezaji na EuroMoney Market Leaders kwa SMEs 2022 zilizotolewa na EuroMoney, Benki ya Stanbic inaendelea kuwa benki ilyodhamiria kuwa sehemu ya kipekee inayochochea ukuaji wa wajasiriamali, kupitia kuwajengea uwezo, ushirikishwaji wa kifedha na kutoa kufadhili ambao ni zaidi ya huduma za kibenki.
MWISHO