Klabu Azam FC imemteua mkufunzi Denis Lavagne (58) kama kocha mkuu klabuni hapo kuchukua mikoba ya Abdihamid Moallin na anatarajiwa kutua Nchini leo Jumanne tayari kwa kuanza majukumu yake.
Lavagne (58) raia wa Ufaransa ni kocha wa viwango vya juu sana akiwa na uzoefu na soka la Afrika, amewahi kufundisha timu ya Taifa ya Cameroon (2011-2012), miamba ya Algeria, USM Alger na JS Kabylie.
Aidha amewahi kufundisha vigogo wa Tunisia, Etoile Du Sahel (2013), Smouha ya Misri, Coton Sports (Cameroon), Al Hilal ya Sudan.
Moja ya mafanikio yake ni kufika fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2008 akiwa na Coton Sport ya Cameroon na kupoteza dhidi ya Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 4-2.
Ubora wa mbinu zake, zilimwezesha mwaka jana, kuiongoza JS Kabylie ya Algeria kushika nafasi ya pili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, ikicheza fainali na Raja Casablanca ya Morocco na kupoteza kwa mabao 2-1.
Mtaalamu huyo ni kocha wa makombe, kwani aliiwezesha Coton Sport kutwaa mataji manne ya ligi (2007, 2008, 2010, 2011), aliiongoza Al Hilal kutwaa taji la ligi mwaka 2016, aliiongoza JS Kabylie kubeba taji la Kombe la FA (2021) na Etoile Du Sahel kutwaa ubingwa kama huo Tunisia mwaka 2013.