Uongozi wa Konde Music Worldwide umeingia mitini baada ya kutakiwa kufika Baraza la Sanaa (Basata) kwenye kikao cha kujadili kuhusiana na sakata la kuwatimua wasanii wao Killy na Cheed kwenye leo.
–
Tukio hilo limetokea jana Jumatano, Oktoba 12, 2022 katika ofisi za Basata Kivukoni jijini hapa ambapo kikao hicho ilikuwa kifanyike. Hilo linatokea ikiwa imepita siku moja tangu uongozi wa lebo hiyo utangaze kuachana na wasanii hao kwa sababu ambazo hawakuziweka wazi.
–
Kutokana na hilo, wasanii waliotimuliwa walifikisha malalamiko yao Basata na kulitakiwa kikae kikao cha pande zote mbili kulizungumzia hilo taarifa ambayo inaelezwa walitaarifiwa kwa njia ya barua pepe (email) lakini mpaka inafika saa nane mchana sio Harmonize wala meneja wake waliotokea katika kikao hicho ambacho kilipaswa kuanza saa sita mchana.
–
Hata hivyo chanzo kimoja kimesema sababu zilizotolewa na kina Harmonize kushindwa kufika kikaoni ni kwamba hawana nafasi kwa kuwa wanasafari kwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya ku ‘shoot’ na kuahidi kwamba wangeweza kufika kikaoni kuanzia Novemba 18, jambo ambalo Basata hawajakubaliana nalo na kutoa amri ya kufika kikaoni wiki ijayo bila kukosa kwa kile walichodai ni kulidharau baraza hilo.