Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema magonjwa yasiyoambukiza bado ni janga katika taifa letu hivyo kuwataka Wataalamu kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ikiwemo kufanya mazoezi, kupunguza matumizi ya vileo kupita kiasi na ulaji unaofaa.
Prof. Makubi amesema hayo, alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Mkoa ya Amana, ambapo alipata fursa ya kuongea Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Amana, Mwananyamala, Temeke, Tumbi, Mbagala Rangitatu, Kigamboni walioongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume na pamoja na tkamati za usimamizi za afya za Halmashauri.
Amesema, Watanzania wengi wana changamoto za magonjwa ya moyo, kansa, magonjwa ya njia ya hewa, ajali, vyote vinasababisha mzigo mkubwa wa matibabu kwa wananchi na Serikali kwa ujumla, hivyo nguvu ya ziada ya kupeleka elimu kwa jamii inatakiwa.
“Watanzania wengi wana changamoto za magonjwa ya moyo, kansa, magonjwa ya njia ya hewa, ajali, vyote vinasababisha mzigo mkubwa wa matibabu kwa wananchi na Serikali kwa ujumla.”Amesema Prof. Makubi.
Aidha, Prof. Makubi amewaagiza Wataalamu wa afya kuboresha uandikaji wa taarifa za mgonjwa pindi wanapo mhudumia ili kuimarisha ufuatiliaji mzuri wa mgonjwa kwa Mtaalamu anaefuata hivyo kuongeza ufanisi katika kutoa huduma, lakini pia itasaidia Serikali katika kufanya tafiti.
Sambamba na hilo, amewaelekeza viongozi wa Hospitali kuimarisha mifumo ya ICT katika maeneo ya kutolea huduma, ikiwemo kuwa na hatua za mbadala endapo mifumo italeta changamoto ili kuondoa kero za kusubiri muda mrefu na misongamano inayoweza kuzuilika katika maeneo ya utoaji huduma.
Pia, amewaelekeza mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuboresha utendaji kazi katika taasisi hiyo, ikiwemo kufanya malipo ya fedha kwa haraka katika vituo vya kutolea huduma ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa vituo na uboreshaji wa utoaji huduma kwa wananchi.
Hata hivyo, Prof. Makubi ameendelea kuwakumbusha juu ya kuboresha huduma za mama na mtoto ili kupunguza au kuondoa vifo, huku akisisitiza kuendelea kufanyia uchunguzi kwa karibu vifo vyote vinavyotokana na uzazi ili kujua namna bora ya kukabiliana dhidi ya changamoto hiyo katika vituo vya kutolea huduma.
Mwisho.

