
Kambi ya siku tano iliyofanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Mending Kids la nchini Marekani kwaajili ya kuwafanyia upasuaji watoto wenye changamoto za moyo imeleta matokeo chanya kwa taifa kutumia gharama ya kawaida na kuokoa fedha nyingi.
Hivyo kupitia kambi hio maalum ya Madaktari Bingwa hapa nchini imeifanya serikali kupunguza gharama za matibabu kwa watoto waliopata nafasi ya kupewa matibabu hayo.
Kwa watoto hawa kufanyiwa upasuaji huu hapa nchini Serikali imeweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni moja fedha ambazo zingelipwa kama upasuaji huo ungefanyika nje ya nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kati ya watoto 40 waliofanyiwa upasuaji 20 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na 20 walifanyiwa upasuaji kwa njia ya tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab.

Dkt. Kisenge alisema tangu waanze kushirikiana na shirika hilo la Mending Kids jumla ya kambi sita za matibabu ya moyo kwa watoto zimeshafanywa huku wataalamu wa JKCI wakifundishwa njia mbalimbali za kufanya upasuaji wa kufungua kifua na ule wa tundu dogo kwa utaalam zaidi.
“Kupitia Shirika la Mending Kids wataalam wa JKCI wa upasuaji wa moyo kwa watoto wamekuwa mabingwa wabobezi katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo hivyo kutufanya kuwa mabingwa kusini mwa jangwa la Sahara katika kutoa huduma bora za matibabu ya moyo kwa watoto,” alisema Dkt. Kisenge.


ADVERTISEMENT