WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita haitawatupa wakulima wa tumbaku na amewataka waongeze uzalishaji kwani soko la uhakika lipo.
“Serikali yenu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan haitawatupa mkono, nami kwa maelezo yenu ya leo nitamfikishia salamu Mheshimiwa Rais kuwa mmeazimia mtalima zaidi tumbaku,” amesema.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Oktoba 18, 2022) wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku wilayani Namtumbo kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Nasuli, wilayani humo. Wadau hao wanajumuisha wakulima, wanunuzi, wenye viwanda, maafisa kilimo, wasambazaji mbolea na wenye mabenki.
Waziri Mkuu amewapa maagizo viongozi wa mkoa na wilaya wahakikishe kuwa pembejeo za kilimo zinazotolewa na Serikali kwa njia ya ruzuku zinawafikia walengwa na hakuna ubadhirifu unaofanywa.
Akitoa maelekezo kwa viongozi wa mkoa wa Ruvuma, amewataka washirikiane na Wizara ya Kilimo kusimamia upatikanaji wa huduma za ugani kwa wakati ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija. “Maafisa Kilimo walio chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI na wale walio Wizara ya Kilimo waratibiwe na kusimamiwa kwa pamoja ili wafanye kazi ya kuwahudumia wakulima kwa ufanisi,” amesisitiza.
Akitoa maelekezo kwa Bodi ya Tumbaku, Waziri Mkuu ametaka kuwepo na mikakati madhubuti ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo ili kufikia malengo yaliyowekwa na kusisitiza kuwa wakulima wa tumbaku waelimishwe kufuata mbinu bora za kilimo ili wazalishe kwa tija.
“Bodi ya Tumbaku isimamie upatikanaji wa pembejeo na kuhakikisha zinawafikia wakulima kwa wakati. Kwa kuwa msimu wa uzalishaji wa tumbaku umeanza, pembejeo katika zao hilo ziharakishwe kuwafikia wakulima,” amesisitiza.
Kuhusu malipo kwa wakulima wa zao hilo, Waziri Mkuu ametaka usimamizi wa malipo ya wakulima uimarishwe ili wakulima walipwe kwa wakati. “Masoko ya uuzaji wa tumbaku yaimarishwe sambamba na kutatua changamoto zilizopo ili wakulima wa tumbaku wapate tija zaidi,” ameongeza.
ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT