Wamiliki wa nyumba nchini Qatar wamekuwa wakipandisha kodi kwa kasi kubwa kuelekea Kombe la Dunia 2022 linalotarajia kuanza mwezi ujao.
–
Wapangaji wa nyumba wengi wao wakiwa ni raia wa kigeni wamekuwa wakiombwa kulipa pesa zaidi au kuhama ili ziwekwe sokoni kwa ajili ya mashabiki wa soka.
–
Zaidi ya mashabiki milioni moja wanategemewa kwenda Jijini Doha kati ya mwezi Novemba na Desemba wakati wa Mashindano hayo, jambo ambalo litakuwa ni mzigo mkubwa kwa nchi ndogo kama Qatar.
–
Mpangaji mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema “baadhi ya wamiliki wa nyumba hawana huruma na wamefikia hatua ya kutoa notisi ya muda mfupi sana ili waweze kupangisha watu watakaowalipa pesa nyingi zaidi,”
–
“Nimeishi kwenye lile jengo kwa miaka miwili na nimekuwa nikilipa kodi ya dola za Kimarekani 2500 kwa mwezi, mwenye nyumba aliniambia niongeze pesa au nihame ndani ya wiki moja. Nyumba hiyo itagharimu dola 1700 kwa usiku mmoja kuanzia mwezi ujao, sikuweza bei hiyo, nilihama.”