
Serikali imeziagiza Mamlaka za usafirishaji abiria Jijini Dodoma kuhakikisha daladala zote zinaanzia sokoni Machinga Complex ili kuongeza hadhi ya soko na kuinua uchumi wa Wafanyabiashara.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alipofanya ziara katika soko la Machinga Complex eneo la Bahi Road Jijini Dodoma tarehe 24 Novemba, 2022 kujionea maendeleo ya soko hilo pamoja na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao wadogo.
“mabasi kutoka pande zote yanayokwenda Ihumwa, UDOM, Kisasa, Msalato, yaanzie hapa, ni agizo nataka nione yanatekelezwa hayo, nikimaliza hapa Jiji na LATRA muondoke mkae, mzungumze na wafanyabiashara na wamiliki wa mabasi madogo muwaelekeze mtengeneze route (safari) ianze tuone mabasi yakiingia hapa” alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Aidha, Mhe. Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi wa jiji la Dodoma kufanya vikao vya pamoja na Wafanyabiashara wadogo hao ili kufikia hatua ya makubaliano kuhusu malipo ya ushuru wa kufanya biashara katika soko hilo badala ya kuanza kutoza viwango ambavyo vitaamuliwa na upande mmoja wa Serikali.
Pia Waziri Mkuu Majaliwa amemwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kuwanyang’anya vibanda watu 28 ambao walipata vibanda viwili badala ya kimoja ili vibanda 28 wagawiwe wafanyabiashara waliokosa vibanda sokoni hapo.
Mhe. Dkt. Festo Dugange Naibu Waziri (AFYA) Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema soko hilo ni moja ya masoko 11 ambayo ni matokeo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka wafanyabiashara hao wafanyebiashara zao katika mazingira salama ili wasihangaike kwenye jua, mvua na vumbi wakiwa hali wakitembea barabarani.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Bw. Joseph Mafuru amesema soko hilo limegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 9 (9,529,747,200) ikiwa shilingi Bilioni 6.5 ni fedha za mapato ya ndani, Bilioni 2.5 ruzuku kutoka Serikali Kuu na milioni 500 fedha za Uviko 19 kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Naye Bw. Christine Msumari Kiongozi wa Wafanyabiashara ndogo ndogo katika soko la Machinga Complex amemwomba Mhe. Waziri Mkuu kuangalia namna ya kuwapatia mikopo wafanyabiashara hao bila ya kuangalia umri ambao ni kikwazo kwa baadhi ya wafanyabiashara kwani unamtambua kijana ni yule asiyezidi miaka 35.


ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT