Imeelezwa kwamba asilimia 40 ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kimwili au kingono mara moja au zaidi katika kipindi cha maisha yao.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima, ameyasema hayo akizungumza na waandishi wa Habari pamoja na wananchi katika soko la Kigogo Fresh, Pugu jijini Dar es Salaam tarehe 22 Novemba, 2022 kuelekea siku 16 za kupinga ukatili.
Waziri Dkt. Gwajima amesema taarifa hizo za Utafiti wa Afya ya uzazi na Viashiria vya Malaria inaonesha pia kwa mwaka 2015/16 kwamba asilimia 20 ya wanawake wa umri huo wameingiliwa kimwili bila ridhaa yao.
“Katika kupambana na tatizo la Mauaji na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, jamii yote tunatakiwa kuunganisha nguvu kwenye kubuni mikakati ya kijamii ambayo italeta tija na suluhisho la kudumu. Kwenye maeneo mengi ya nchi kuongezeka kwa uelewa juu ya masuala ya ukatili na madhara yake ni kutokana na utekelezaji wa mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Mwaka 2017/18-2021/22 (MTAKUWWA)” amesema Dkt. Gwajima.
Amebainisha kuwa katika mpango wa MTAKUWWA wa miaka mitano, matokeo chanya yamepatikana kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe na hasa kuwahusisha viongozi wa kijamii wakiwemo viongozi wa dini, viongozi wa kimila, wazee maarufu na watu wengine ambao wana sauti ndani ya jamii.
Ameongeza kwamba, katika kukabiliana na vitendo vya Ukatili wa Kijinsia hapa nchini, Serikali kwa kushirikian na wadau, imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili.
Waziri Dkt. Gwajima amewataka wanaume kujitokeza kushiriki kutokomeza vitendo vya ukatili hasa kwa upande wao badala ya kuchukua maamuzi ambayo yana madhara kwa familia na jamii kwa ujumla.
“Serikali kupitia Wizara hii inashughulikia jinsia zote kwa ngazi zote kuanzia Polisi, Magereza, Halmashauri na pia namba 116, elezeni changamoto zenu” ameongeza Waziri Gwajima.
@gwajimad @ortamisemi @wildaftz @16daysofactivismcampaign_tz

ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT