
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali yenye lengo la kuhakikisha asilimia 60 ya korosho zote zinazozalishwa nchini zinabanguliwa ifikapo msimu wa mwaka 2025/2026.
Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo tarehe 31 Novemba, 2022 akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokuwa akishuhudia tani 7.5 za korosho zilizoongezwa thamani ukisafirishwa kwenda katika soko la kimataifa nchini Marekani na kampuni ya Ward Holding Tanzania (WHT).
“Leo tunashuhudia tukio la kihistoria, ambapo korosho iliyobanguliwa nchini Tanzania inaenda kuuzwa kwa mtumiaji wa mwisho nchini Marekani. Hii ni habari njema kwa wakulima wa korosho nchini na ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu mpendwa Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kufungua nchi kimataifa, hali inayopelekea kuongeza uhakika wa masoko ya mazao ya wakulima wetu.
Bei ya korosho ghafi nchini ni kati ya 1,800 hadi 2,200 ambapo unahitaji kilo tano za korosho ghafi ili kupata kilo moja ya korosho iliyobanguliwa. Wakati huo huo, bei ya korosho iliyobanguliwa nchini Marekani ni Dola za Kimarekani 40 (sawa na zaidi ya shilingi 90,000 za Kitanzania), hesabu hii inaonesha dhahiri kuwa kuuza korosho iliyobanguliwa kuna manufaa makubwa kwa wakulima wetu na Taifa kwa ujumla.
Wizara ya Kilimo inatekeleza mpango wake wa Ajenda 10/30 wenye lengo la kuhakikisha kilimo kinakua kwa wastani wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, msukumo mkubwa kufikia lengo hilo upo katika upatikanaji wa masoko ya uhakika ambayo yatamvutia mkulima kulima kwa tija na faida.
Kila kitu katika bidhaa hii, kuanzia kuibangua na kuiweka kwenye vifungashio vinavyovutia imefanywa hapa hapa Tanzania.Nitoe rai kwa Taasisi za fedha kuendelea kuunga mkono juhudi za wajasiriamali na sekta binafsi kwa ujumla.”Alisema Naibu Waziri Mavunde.
Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania,Mhe. Robert Raines ameihakikishia Tanzania ushirikiano wa kutosha ili kuwawezesha wakulima wa korosho kupata soko la uhakika nchini Marekani.
@anthonymavunde @bashehussein
#Ajenda10/30

ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT