Benki ya NBC Yazindua Hati Fungani ya NBC Twiga ili kuwainua wajasiriamali na wadau wa kilimo.
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imetangaza utoaji wa Dhamana (bondi) ya miaka mitano (5) inayofahamika kama Dhamana ya Twiga NBC, (NBC Twiga Bond) ambayo inamlenga mtu yeyote anayetaka kuwekeza na kupata faida nzuri.
Kiasi cha chini cha ununuzi wa dhamana hiyo ni TZS 500,000 na inaweza kununuliwa kutoka tawi lolote la Benki ya NBC, au Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) wenye leseni ya Dalali.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi alisema, “Kama mmoja wa wakopeshaji wakubwa nchini Tanzania, tunayofuraha kutoa Dhamana yetu (bondi) ya kwanza sokoni iliyopewa jina la Dhamana ya Twiga NBC (NBC Twiga Bond) tukilenga kuongeza TZS300Bn ambazo zitatumika katika kufadhili sekta ndogo na za kati, Kilimo na sekta nyinginezo muhimu kiuchumi nchini.
Mapato yatokanayo na Dhamana ya Twiga yatatuwezesha kukidhi mahitaji ya kifedha kwa ajili ya makundi haya muhimu ambayo yanaajiri watu wengi. Dhamana ya Twiga NBC iko wazi kwa umma, tukimaanisha zinaweza kununuliwa na watu binafsi, makampuni na taasisi. Ni matumaini yetu kuwa hatua hii itakuza ufanisi wa uzalishaji, kuongeza ushindani wa soko, na kutetea kanuni bora za utawala na uwajibikaji katika shughuli za biashara,” alisema.