Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kamishna Jenerali John Masunga amesema kuwa kijana Majaliwa Jackson Samweli, ameshapokelewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Hivyo maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Samia Suluhu Hassan tayari yameshatekelezwa.
–
Majaliwa anatarajiwa kuanza mafunzo ya Zimamoto na Uokoaji pamoja na ya Uaskari katika Chuo cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kilichopo Chogo Wilaya ya Handeni Mkoa wa Tanga.
–
Ikumbukwe kuwa tarehe 06 Novemba, 2022 ilitokea ajali ya kuanguka kwa Ndege ya Precision Air katika Ziwa Victoria, ajali hiyo ilisababisha majeruhi na vifo. Majaliwa alionesha ujasiri wa hali ya juu kwa kuokoa wahanga 24 wa tukio hilo.
–
Kamishna Jenerali Masunga ametoa shukrani za dhati kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Taasisi za Umma na Binafsi, pamoja na Wananchi wa Mkoa wa Kagera kwa ushirikiano mkubwa waliotoa katika zoezi la uokoaji katika ajali hiyo.
–
Aidha ametoa pole kwa Wafiwa wote na kuwaombea faraja katika kipindi hiki kigumu wanachopitia na amewatakia majeruhi wote afya njema.
–
Kamishna Jenerali Masunga amewasihi Wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kuokoa Maisha ya watu na mali dhidi ya majanga mbalimbali