Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha ujenzi wa shule ya wasichana Kitaifa inayojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe unakamilika ifikapo Desemba 30, 2022.
Akiongea na Viongozi wa Mkoa wa Kagera, Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Wakandarasi na baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Rais TAMISEMI wakati wa kikao hicho ofisini kwake Jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI) Mheshimiwa Angela, amewaagiza Viongozi hao kuhakikisha ujenzi wa shule hiyo ya bweni ya wasichana wilayani Karagwe unakamilika ndani ya muda uliopangwa ambao ni Desemba 30, 2022.
Waziri Kairuki amefanya kikao hicho ili kuweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
“napenda pia nipate taarifa ya uendelevu wa ujenzi wa majengo hayo ya shule ya sekondari kwa kila hatua, kila mwisho wa wiki, mimi nawashukuru tukatekeleze mikakati tuliyokubaliana” amesema Waziri Kairuki.
Kikao hicho kimekuja kufuatia kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) chini ya Mwenyekiti wake Abdallah Chaurembo kilichopitia utekelezaji wa ujenzi wa shule mpya za sekondari unaotekelezwa chini ya Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) na kubaini kuwa ujenzi wa shule ya bweni ya wasichana Kitaifa inayojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe hauridhishi na hivyo Serikali ni lazima ichukue hatua za haraka kukamilisha malengo yaliyowekwa.